Haijuzu kwa mtu kuichelewesha mpaka wakati wa kuswaliwa ´iyd. Akiichelewesha baada ya kuswaliwa ´iyd pasi na udhuru haikubaliwi, kwa sababu ni kwenda kinyume na yale aliyoamrisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) imeshatangulia kwamba mwenye kuitoa kabla ya kuswaliwa basi hiyo ni zakaah yenye kukubaliwa, na mwenye kuitoa baada ya kuswaliwa ni swadaqah miongoni mwa swadaqah zingine.

Lakini hapana neno akiichelewesha kutokana na udhuru. Kwa mfano siku ya ´iyd imkute akiwa nyikani na hana chakula cha kutoa au hakuna mtu wa kumpa chakula hicho. Hali nyingine ni kwamba taarifa ya kwamba ni ´iyd imemfikia ghafla kwa namna ya kwamba hawezi kuwahi kuitoa kabla ya swalah. Hali nyingine ni kwamba akamuwakilisha mtu amtolee ambapo mtu huyo akasahau kuitoa. Hapana vibaya kuitoa, ijapo ni baada ya ´iyd, kwa sababu ni mwenye kupewa udhuru kwa jambo hilo.

Ni wajibu iwafikie ambao wanaiistahiki au mwakilishi wake kabla ya swalah. Endapo mtu atamkusudia kumpa mtu fulani na asimpate mtu huyo wala yule mwakilishi wake kipindi cha kutolewa kwake, basi ampe nayo mtu mwingine mwenye kuiistahiki na wala asiicheleweshe nje ya wakati wake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 212
  • Imechapishwa: 24/03/2024