97. Hakuna muislamu yeyote anayekufuru kwa maasi

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuna yeyote katika watu wa Qiblah anayekufuru kwa dhambi.

MAELEZO

Huu ni msingi miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah; madhambi yote chini ya shirki na maasi yameharamishwa na juu yake kuna matishio, lakini mwenye nayo hafiki kwenye kiwango cha ukafiri ambapo akatoka nje ya Uislamu muda wa kuwa anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, anaswali, anatoa zakaah, anafunga Ramadhaan na anahiji katika Nyumba.

Madhambi mbali na shirki na kufuru yamegawanyika mafungu mawili: madhambi makubwa na madhambi madogo. Madhambi makubwa na madogo hayapelekei katika ukafiri wenye kumtoa mtu nje ya Uislamu. Hapana shaka kwamba madhambi yanaweza kuitwa kufuru ndogo, lakini Khawaarij peke yao ndio wenye kuwakufurisha waislamu kwa kutenda dhambi kubwa na wanawahukumu kwamba watadumishwa Motoni milele. ´Aqiydah yao ni batili. Kwa ajili hiyo wanawakufurisha Ahl-us-Sunnah, wanawapiga vita na wanamwaga damu na kupora mali zao. Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaona kuwa maasi yanaipunguza imani, lakini hata hivyo hayamtoi mwenye nayo nje ya Uislamu, kama ilivyofahamisha Qur-aan na Sunnah.

Murji-ah wameonelea kinyume na Khawaarij ambao wanaona kuwa imani ni kule kusadikisha kwa moyo. Hoja wanayotoa ni kwamba midhali mtu ni mwenye kusadikisha kwa moyo wake basi ni muumini. Kwa vile matendo hayaingii katika imani, basi hadhuriwi na maasi, sembuse yakamfanya kuwa kafiri. Wanasema kuwa imani haidhuriki kwa kuwepo maasi kama ambavo utiifu haunufaishi kwa kuwepo kufuru. Ni kweli na sahihi kwamba utiifu haunufaishi kwa kuwepo kufuru lakini si sawa wala sahihi kwamba imani haidhuriki kwa kuwepo maasi. Muumini maasi yake ni yenye kumdhuru ingawa si yenye kumtoa nje ya Uislamu. Lakini hata hivyo yanamdhuru na yanaweza kumfanya hata akaadhibiwa ndani ya Moto. Watenda madhambi makubwa wakitubu, basi Allaah huwasemehe. Na wasipotubu basi wako chini ya utashi wa Allaah; akitaka atawasamehe na akitaka atawaadhibu kwa kiwango cha madhambi yao. Kisha baadaye watatolewa nje ya Moto kutokana na imani yao. Wanaweza kubaki Motoni kwa kipindi kirefu, lakini pale mwanzoni tu au mwishoni wakatoka nje ya Moto kwa idhini ya Allaah, wakatoka ima kwa uombezi wa waombezi, kumalizika kwa adhabu yao au pia kwa rehema za Allaah. Kwa hali yoyote ile mafikio yao ya mwisho ni Peponi, kama zilivyojulisha dalili Swahiyh. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Allaah ndiye mwenye kuamua nini cha kuwafanya watenda madhambi makubwa. Akitaka kuwasamehe atawasamehe na akitaka kuwaadhibu atawaadhibu kisha baadaye awaingize Peponi. Kuna uwezekano vilevile wakaadhibiwa kwa majanga mbalimbali ya duniani. Kwa msemo mwingine ni kwamba maasi yanadhuru na kuipunguza imani na kwa ajili hiyo mtu asiyachukulie wepesi. Lakini hayaungwi chumvi kiasi cha kwamba yanamtia ukafirini mwenye nayo na kumdumisha Motoni milele, kama wanavosema Khawaarij. Madhehebu yote mawili ni batili. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio ya kati na kati, ya kati na kati baina ya madhehebu mbili batili, haki baina ya ´Aqiydah mbili potofu. Khawaarij wanatendea kazi maandiko ya adhabu na matashio na Murji-ah wanatendea kazi maandiko ya ahadi na msamaha. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanatendea kazi maandiko yote mawili na kusema kuwa Allaah ndiye mwamuzi wa kufanya akitakacho.

[1] 04:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 74-75
  • Imechapishwa: 26/08/2021