96. Tofauti ya mavazi ya wanaume na mavazi ya wanawake

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Ni jambo linalotambulika kuwa majumba ni aina moja wapo ya mavazi. Yote mawili yamefanywa kwa ajili ya ulinzi na kuondosha madhara, kama ambavo chakula na kinywaji vimefanywa kwa ajili ya kuleta manufaa. Mavazi yanamlinda mtu kuzuia joto na baridi na silaha ya adui, majumbani yanalinda kutokana na joto na baridi na adui. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّن بُيُوتِكُمْ سَكَنًا

”Allaah amekufanyieni majumba yenu kuwa maskani.”[1]

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّمَّا خَلَقَ ظِلَالًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنَ الْجِبَالِ أَكْنَانًا وَجَعَلَ لَكُمْ سَرَابِيلَ تَقِيكُمُ الْحَرَّ وَسَرَابِيلَ تَقِيكُم بَأْسَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُتِمُّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْلِمُونَ

”Allaah amekufanyieni vivuli katika alivyoumba na akakujaalieni katika milima mapango na amekujaalieni mavazi yanakukingeni na joto na mavazi yanakukingeni katika vita vyenu. Namna hiyo ndivo anavyotimiza neema Yake juu yenu ili mpate kujisalimisha.”[2]

Hapa ametaja yale ambayo watu wanayahitaji ili kujilinda na yale yanayoweza kuwadhuru. Mwanzoni mwa Suurah ametaja yale wanayoyahitaji ili kujilinda na yale yanayowadhuru na akasema:

وَالْأَنْعَامَ خَلَقَهَا ۗ لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُون

”Wanyama hoa amewaumba. Katika hao mna vifaa vya kutia joto na manufaa mengineyo na wengine mnawala.”[3]

Akataja yale wanayotumia ili kujilinda na baridi, kwa sababu baridi inaua na joto linakera. Ndio maana baadhi ya waarabu wakasema kuwa baridi ni tabu na joto ni dhara. Kutokana na sababu hiyo kujilinda na baridi hakukutajwa katika ile Aayah nyingine – kumetajwa mwanzoni. Mwanzoni mwa Suurah kumetajwa msingi wa neema na ukamilifu wake haukutajwa katikati ya Suurah. Kwa ajili hiyo Akasema:

كَذَٰلِكَ يُتِمُّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْلِمُونَ

”Hivyo ndivyo Anavyotimiza neema Yake juu yenu ili mpate kujisalimisha.”

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba malengo ya mavazi yanafanana na malengo ya makazi. Katika mazingira haya wanawake wameamrishwa kujisitiri na kujifunika. Kwa hivyo ikiwa nguo za wanawake na wanaume zinatofautiana, basi wanawake watapaswa kuvaa zile ambazo zinasitiri na kufunika zaidi na nguo za wanaume zitakuwa kinyume chake. Msingi wa hilo ni kwamba Mwekaji Shari´ah ana malengo mawili. Ya kwanza ni kutofautisha kati ya wanaume na wanawake. Ya pili ni wanawake kujisitiri. Ingelikuwa malengo ni kujisitiri peke yake, basi malengo hayo yangelifikia kwa njia yoyote ile, jambo ambalo maharibifu yake yamekwishatangulia.”[4]

[1] 16:80

[2] 16:81

[3] 16:5

[4] al-Kawaakib (93/132-134) ya Ibn ´Urwah al-Hanbaliy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 24/10/2023