2- Wakati wa usiku. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtaja bwana mmoja katika Maswahabah zake ambaye alifariki, akavikwa ndani ya sanda isiyokuwa ndefu na akazikwa usiku, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakemea kuzikwa mtu wakati wa usiku mpaka kwanza aswaliwe. Isipokuwa ikiwa kama mtu atadharurika kufanya hivo.”

Ameipokea Muslim na wengineo. Imekwishatangulia katika masuala 35, uk. 56.

Hadiyth ni yenye kutoa dalili ya wazi kabisa juu ya tuliyoyataja. Pia ndio madhehebu ya Ahmad (Rahimahu Allaah) katika moja ya mapokezi yake. Yametajwa katika “al-Inswaaf” (02/547) ambapo akasema:

“Halifanyiki hilo isipokuwa kwa dharurah.” Katika upokezi wake mwingine amesema: “Imechukizwa.”

Maoni ya kwanza ndio yaliyo karibu zaidi na usawa kutokana na udhahiri wa maneno yake:

“Amekemea.”

Hakika ni yenye nguvu zaidi kuliko tamko la kusema: “Amekataza” ambayo yanaweza kufasiriwa machukizo. Pamoja na kwamba msingi wake ni uharamu na hakuna chenye kuyageuza na kuyapeleka katika machukizo.

Lakini yale tuliyoyataja yanatiwa utata na maneno yake katika Hadiyth:

“… mpaka kwanza aswaliwe.”

yanafahahamisha kwa udhahiri wake pia kufaa kuzika usiku baada ya kumswalia. Kwa sababu kitendo hicho ndio lengo la makatazo. Lipatikana lengo hilo basi kutaondoka makatazo. Lakini yanajiliwa pia na maneno yake:

“Isipokuwa ikiwa kama mtu atadharurika kufanya hivo.”

Hakika jina hilo la kuashiria linarejea katika kile kilichokatazwa, ambacho ni kuzika wakati wa usiku kwa sababu nyingi, kama itavyokuja kutoka kwa Ibn Hazm. Lakini sisi hatufikirii kwa njia yoyote ile kwamba watu wanaweza kulazimika kumzika pasi na kumswalia.

Katika yale yenye kuliongezea umbali ni kwamba maana hii itafanya kile kidhibiti cha “usiku” kutokuwa na faida. Kwani kuzikana kabla ya kuswalia, kama ambavo haifai kufanya hivo wakati wa usiku, vivyo hivyo haifai kufanya hivo mchana. Ikiwa itafaa kufanya hivo usiku kutokana na dharurah basi pia itafaa kufanya hivo mchana kwa ajili yakee na wala hakuna tofauti. Vinginevyo katika hali hiyo kuna faida gani ya kuleta “usiku”? Hapana shaka kwamba faida haitodhihirika kwa sura yenye nguvu isipokuwa pale ambapo tutaanza kukipa nguvu kile tulichoonelea cha kutokufaa kuzika usiku. Ubainifu wa hayo: ni kwamba kuzika wakati wa usiku ni katika yale ambayo dhana inapelekea uchache wa waswaliji kwa maiti. Hivyo ndipo akakataza kuzikana usiku ili aswaliwe mchana. Wakati wa mchana watu wanakuwa na uchangamfu wa kumswalia. Kwa hilo ndipo kutapatikana wingi wa wenye kumswalia. Wingi huu ambao ni moja katika malengo ya Shari´ah na pia unatoa matarajio makubwa zaidi ya kukubaliwa maombezi yao juu ya maiti, kama ilivyotangulia kubainishwa katika masuala ya 63, uk. 96.

an-Nawawiy amesema katika “Sharh Muslim”:

“Kuhusu makatazo ya kuzikana usiku mpaka kwanza aswaliwe, imesemekana kwamba sababu yake ni kuwa kuzikana wakati wa mchana watu wengi wanahudhuria na kumswalia, jambo ambalo halipatikana usiku isipokuwa watu wachache. Pia imesemekana kwamba wao walikuwa wakifanya hivo kutokana na ubaya wa sanda na hivyo haiwezi kuonekana wakati wa usiku, jambo ambalo linatiliwa nguvu na mwanzoni na mwishoni mwa Hadiyth. al-Qaadhwiy amesema:

“Sababu zote mbili ni sahihi. Kilicho dhahiri ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameyakusudia yote mawili kwa pamoja. Lakini yapo mengine pia yaliyosemekana.”

Ikishatambulika kuwa sababu ni uchache wa waswaliji na kukhofia ubaya wa sanda basi kunazalikana kutokana na hayo kwamba endapo ataswaliwa wakati wa mchana kisha akachelewa kuzikwa kwa sababu ya udhuru mpaka ukaignia wakati wa usiku kwamba hakuna kizuizi kwa kuondoka kile kikwazo na  kupatikana kwa lengo ambalo ni wengi wa waswaliji.

Kutokana na hayo inafaa kuchelewesha kumzika maiti mchana kwa sababu ya kupatikanisha hilo lengo lililotajwa? as-Swa´aaniy ameliona kuwa zuri hilo katika “Subul-us-Salaam” (02/166). Lakini mimi sioni kufaa kufanya hivo kwa kuwa sababu iliyotajwa imedhibitiwa na wakati wa usiku. Hivyo haijuzu kuuruka mpaka wakati wa mchana kwa sababu ya kupatikana tofauti kubwa baina ya hali hizo mbili. Uchache unaopatikana wakati wa usiku ni jambo la kimaumbile kinyume na mchana ambapo wingi ndio jambo la kimaumbile. Jengine ni kwamba wingi huu hauna kikomo. Kila ambavo maiti atavyochelewesha zaidi basi wingi utazidi. Kwa ajili hiyo tunawaona baadhi ya watu wenye mali ambao wanapenda kuonekana kwa lengo la kujionyesha na kutaka kusikika – ijapo ni kwa hesabu ya maiti – wanaweza kumchelewesha siku moja au mbili ili mazishi yaweze kuhudhuriwa na idadi kubwa iwezekanayo. Lau itasemwa kuwa kufanya hivo inafaa basi itapelekea kukinzana na mwenye Shari´ah katika amri Yake ya kufanya haraka kumwandaa maiti kwa yale yaliyotangulia ubainifu wake katika masuala ya 17, uk. 13, kwa sababu ya wingi usiokuwa na kidhibiti.

Baada ya haya yote kutabainika majibu juu ya ule utata niliyoutaja katika maneno yake:

“… mpaka kwanza aswaliwe.”

Kwa sababu imekwishadhihi kwamba makusudio ni mpaka aswaliwe wakati wa mchana kutokana na wingi wa watu. Ili uweze kubainisha kuwa jina la ishara katika maneno yake:

“Isipokuwa ikiwa kama mtu atadharurika kufanya hivo.”

linarejea kuzikana wakati wa usiku ijapo ni idadi chache ya wenye kuswali. Hakumaanishwi kuzikana pamoja na kuacha kumswalia kabisa. Hilo linahitaji kuzingatiwa! Ndilo la haki kwa mazingatio.

Kisha an-Nawawiy akasema katika “Sharh Muslim”:

“Wanachuoni wametofautiana juu ya kuzika usiku. al-Hasan al-Baswriy amelichukiza hilo isipokuwa kwa dharurah. Hadiyth hii ni miongoni mwa anayoyajengea hoja. Jopo la wanachuoni wengi katika wale waliotangulia na wale waliokuja nyuma wakasema kuwa haikuchukizwa. Wamejengea hoja kwamba Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) na kikosi katika Salaf walizikwa wakati wa usiku bila kuwepo kwa makemeo, mwanamke cheusi na yule mtu ambaye alikuwa akifanya kazi msikitini akafariki na kuzikwa usiku ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwauliza juu yake ambapo wakajibu kwamba amekufa usiku na wakamzika usiku. Akawauliza ni kwa nini hawakumjuza ambapo wakajibu kuwa kulikuwa na giza. Hakuwakaripia. Wamejibu kuhusu Hadiyth hii kwamba makatazo yalikuwa kwa kuacha kumswalia na wala haikukatazwa kitendo cha kuzika usiku. Isipokuwa ni kwa sababu ya kuacha kuswaliwa, kwa sababu ya uchache wa waswaliji, ubaya wa sanda au yote hayo kama ilivyotangulia.”

Jibu la kwanza – kwamba makatazo yalikuwa kwa kuacha kumswalia – si sahihi. Kwa sababu mambo yangelikuwa hivo basi kusingelikuwa na tofauti kati ya kuzika usiku na kuzika mchana, kama ilivyotangulia kubainishwa. Bali usawa ni kwamba makatazo yalikuwa kwa mambo mawili ambayo yametangulia katika maneno ya al-Qaadhwiy. Kwa ajili hiyo Ibn Hazm amechagua kuwa haijuzu kumzika yeyote wakati wa usiku isipokuwa kutokana na dharurah. Amejengea juu ya hayo kwa Hadiyth hii. Halafu akajibu kuhusu Hadiyth iliyopokelewa juu ya kuzika usiku na mapokezi yaliyokuja kwa maana kama hiyo katika “al-Muhallaa” (05/114-115):

“Kila ambaye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimzika usiku katika wakeze na Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum) ni kutokana na dharurah iliyopelekea kufanya hivo katika kuchelea joto kali kwa wale wahudhuriaji – jambo ambalo ni kali katika mji wa al-Madiynah – kuchelea kugeuka au mengineyo katika ambayo yanahalalisha kuzika wakati wa usiku. Haimstahikii yeyote kuwafikiria (Radhiya Allaahu ´anhum) kinyume na hivo.”

Kisha akataja machukizo ya kuzika usiku kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyib.

Miongoni mwa mambo yanayofaa ni kwamba baadhi ya waliozikwa usiku waliswaliwa kipindi cha mchana. Hivyo basi kutakuwa hakuna mgongano katika yale tuliyotangulia  kuyabainisha, jambo ambalo ndio uhalisia juu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walimswalia siku ya jumanne kisha wakamzika siku ya jumatano. Hayo yametajwa na Ibn Hishaam katika “Siyrah” yake (04/314) kutoka kwa Ibn Ishaaq. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 176-180
  • Imechapishwa: 16/02/2022