Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

Kuamini mipango na makadirio ndani yake kuna ngazi nne ambazo ni zifuatazo:

1 – Allaah ameyajua mambo milele. Aliyajua yaliyokuwepo na yatayokuwepo na ambayo hayapo endapo yangelikuwa namna gani. Hakuna chochote kinachofichikana Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala).

2 – Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameandika makadirio yote katika Ubao uliohifadhiwa. Uandishi huu umekienea kila kitu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika!” Kukadiriwa yote yatayokuwepo hadi siku ya Qiyaamah.”[1]

Kwa hiyo kalamu ikaandika kila kitachokuweko mpaka siku ya Qiyaamah.

3 – Hakuna kinachopitika katika ulimwengu huu isipokuwa kwa matakwa na utashi wa Allaah. Yote tayari yamo katika Ubao uliohifadhiwa, yote hayo anayajua. Hakutokei kitu pasi na matakwa Yake. Hakutokei kitu katika ufalme Wake asichokitaka:

إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

“Hakika Allaah atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema mabustani yapitayo chini yake mito. Hakika Allaah anafanya atakavyo.”[2]

كَذَٰلِكَ اللَّـهُ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ

“Hivo ndivyo Allaah hufanya atakavyo.”[3]

Kila kinachotokea katika ulimwengu huu – kukiwemo uhai na kifo, utajiri na umasikini, imani na ukafiri – yote hayo ni kwa sababu Allaah ametaka yatokee. Ametaka kheri na shari, imani na kufuru. Kila kitu kinaingia ndani ya utashi Wake; anayoyataka, hutokea, na asiyoyataka, hayatokei.

4 – Allaah anaumba. Anapotaka kitu kiwepo, basi anakiumba:

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

”Allaah ni Muumbaji wa kila jambo, Naye juu ya kila jambo ni mdhamini.”[4]

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.”[5]

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

 “Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla Hatujauumba.”[6]

Kuna Aayah nyingi kama hizo.

[1] Ahmad (5/317), Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (1/48).

[2] 22:14

[3] 3:40

[4] 39:62

[5] 7:54

[6] 57:22

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 106-107
  • Imechapishwa: 29/10/2024