91. Nyusiku ambazo unapatikana usiku wa makadirio

Usiku wa makadirio unakuwa ndani ya Ramadhaan, kwa sababu Allaah ameiteremsha Qur-aan ndani yake. Amekhabarisha kuwa kuiteremsha Kwake ni katika mwezi wa Ramadhaan. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ

“Hakika Sisi Tumeiteremsha katika usiku wa Qadar.”

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُوَالْفُرْقَانِ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan.”[1]

Kutokana na haya imelazimika usiku wa makadirio uwe ndani ya Ramadhaan. Usiku huo uko katika nyumati zingine pia na katika ummah huu pia mpaka siku ya Qiyaamah. Imaam Ahmad na an-Nasaa´iy wamepokea kupitia kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Ee Mtume wa Allaah, nipe khabari kuhusu usiku wa makadirio! Uko ndani ya Ramadhaan au wakati mwingine?” Akasema: “Bali uko ndani ya Ramadhaan.” Akauliza tena: “Unakuwa pamoja na Mitume muda wa kuwa wapo; wanapofishwa unanyanyuliwa au unakuwepo mpaka siku ya Qiyaamah?” Akasema: “Bali unakuwepo hadi siku ya Qiyaamah.”[2]

Hata hivyo fadhilah na ujira wake – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni maalum kwa ummah huu kama ambavo fadhilah za siku ya ijumaa zimefanywa kuwa ni maalum juu ya ummah huu.

Usiku wa makadirio unakuwa katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni usiku wa makadirio katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ni karibu zaidi kupatikana katika yale masiku ya witiri kuliko masiku ya shufwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni usiku wa makadirio katika katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan ya witiri.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Ni karibu zaidi kupatikana katika yale masiku saba ya mwisho. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwamba:

“Baadhi ya watu katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliona usiku wa makadirio usingizini katika yale masiku saba ya mwisho. Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Naona ndoto zetu zimeafikiana juu ya yale masiku saba. Kwa hivyo mwenye kuutafuta basi autafute katika yale masiku saba ya mwisho.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Muslim pia amepokea kupitia kwake ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni (yaani usiku wa makadirio) katika zile siku kumi za mwisho. Akidhoofika mmoja wenu au akashindwa basi zisimshinde zile siku saba zilizobakia.”

Siku ambayo ni karibu zaidi kupatikana kwake katika zile nyusiku saba za mwisho ni usiku wa tarehe ishirini na saba. Ubayy bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Naapa kwa Allaah najua ni usiku gani; ni ule usiku ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuusimama; ni usiku wa tarehe ishirini na saba.”

Ameipokea Muslim.

Usiku wa makadirio sio makhsusi usiku maalum miaka yote. Bali unahamahama; kwa mfano mwaka huu unaweza kuwa tarehe 27 na mwaka mwingine unakuwa tarehe 25 kwa mujibu wa matakwa na hekima ya Allaah. Dalili ya hilo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Utafuteni; ni wenye kubaki [usiku wa] wa tisa, ni wenye kubaki wa saba na ni wenye kubaki wa tano.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Amesema [Ibn Hajar] katika “Fath-ul-Baariy”:

“Maoni yenye nguvu ni kwamba ni katika zile nyusiku za mwisho za witiri na kwamba unahamahama.”

[1] 02:185

[2] al-Haakim pia ameipokea na akasema: ”Hadiyth ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim na hakuipokea.”

Imenukuliwa kutoka kwa adh-Dhahabiy kuwa amemkubalia. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 162-163
  • Imechapishwa: 17/03/2024