Haisihi kwa mwanamke mjamzito na mnyonyeshaji kutoa chakula peke yake

Swali: Ni ipi hukumu ya mwanamke mjamzito anapoacha kufunga Ramadhaan kwa kukhofia kipomoko chake na mwanamke anayenyonyesha kwa kuchelea mtoto wake mchanga anayemnyonyesha?

Jibu: Wanazuoni wamekinzana. Miongoni mwao wako waliosema kuwa analazimika kulipa deni lake, wengine wakasema kuwa analazimika kulipa deni lake na kutoa kafara, wengine wakasema kuwa halazimiki kulipa deni lake lakini hata hivo atalazimika kutoa kafara na wengine wakasema kuwa halazimiki kulipa deni lake wala kutoa kafara. Wanajengea hoja kwa Hadiyth ya Anas bin Maalik al-Ka´biy kwamba alifika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye akamwambia: “Kula!” Akajibu kuwa amefunga. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Je, hujui kuwa Allaah amemuwekea msafiri nusu ya swalah na swawm kwa mjamzito na mnyonyeshaji.”

Wamejengea hoja kwa hii kwamba hakuna kinachomlazimu.

Kinachonidhihirikia mimi ni kwamba analazimika kulipa deni lake tu. Kwa msemo mwingine halazimiki kutoa kafara. Haisihi [akitoa chakula peke yake]. Analazimika kulipa deni lake. Amesema (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

[1] 02:184

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaaih wa Naswaaih, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 17/03/2024