90. Mavazi ya wanamme na wanawake wakati wa Mtume

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hakuna kigezo maalum kinachothibitisha namna mavazi yanatakiwa kuonekana, si katika maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala ada ya mavazi ya wanamme na wanawake, kwa kiasi cha kwamba vazi fulani linakuwa wajibu na vazi lingine linakuwa haramu. Kwani hakika wanawake katika wakati wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakivaa mavazi marefu yenye mkia yanayoburuza wakati mwanamke anapotoka nyumbani. Wanamme wameamrishwa kuyapandisha mavazi yao yasivuke kongo mbili za miguu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi basi Allaah hatomwangalia siku ya Qiyaamah.” Umm Salamah akasema: ”Wanawake wafanye nini na mikia yao?” Akasema: ”Waiache ishuke shubiri moja[1].” Akasema: ”Hivyo basi itaonekana miguu yao.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Waiche ishuke dhiraa moja na wasizidishe hapo.”[2]

Kwa sababu hiyo mwanamke ameruhusiwa kuyaburuta mavazi yake juu ya ardhi chafu, yanasafika pindi baadaye anapopita kwenye udongo msafi. Haya ni maoni ya jopo la wanazuoni, akiwemo Ahmad na wengineo. Wanaona kuwa nguo ya mwanamke inayoburutwa ina hukumu moja kama viatu vinavyokanyaga ardhi yenye najisi na baadaye vikasafishwa kwa udongo msafi. Ni kama ambavyo zinasafishwa tupu mbili baada ya kile chenye kutoka.”[3]

[1] Bi maana kuanzia kwenye nusu ya muundi wake. Maoni mengine yanasema kuanzia kwenye vifundo vya miguu.

[2] at-Tirmidhiy (1731), aliyesema kuwa ni nzuri, na an-Nasaa’iy (5338).

[3] al-Kawaakib (93/132-134) ya Ibn ´Urwah al-Hanbaliy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 152-153
  • Imechapishwa: 22/10/2023