Katika Suurah hii kuna fadhilah nyingi za usiku wa makdirio:

1 – Allaah ameiteremsha Qur-aan ambayo ndani yake ndio kuna mwongozo wa watu na kufaulu kwao ulimwenguni na Aakhirah.

2 – Yale yanayofahamishwa na usemi wa kuuliza na kutukuza pale aliposema:

وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ

”Na nini kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadar?”

3 – Ni bora kuliko miezi elfu.

4 – Malaika wanashuka ndani yake. Malaika hawashuki isipokuwa kwa kheri, baraka na rehema.

5 – Amani nyingi kutokana na wingi wa kusalimika kutokana na adhabu kwa sababu ya yale mambo mengi ya utiifu ambayo mja anayafanya kwa Allaah.

6 – Allaah ameshusha kuhusu fadhilah zake Suurah kamili inayosomwa mpaka siku ya Qiyaamah.

Miongoni mwa fadhilah za usiku wa makadirio ni yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesimama usiku wa makadirio hali ya kuwa na imani na matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“… hali ya kuwa na imani… “

Bi maana kumwamini Allaah na zile thawabu alizowaandalia wenye kusimama usiku na akatarajia malipo na kutafuta thawabu. Haya anayapata yule ambaye atajua usiku huo na ambaye hatojua, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufanya kuwa ni sharti kujua usiku huo ili mtu apate ujira huo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 161-162
  • Imechapishwa: 16/03/2024