90. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu kuwasikiliza na kuwatii watawala wa waislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naona ulazima wa kuwasikiliza na kuwatii watawala wa waislamu – ni mamoja ni wema au waovu – muda wa kuwa hawajaamrisha kumuasi Allaah. Yule ambaye atatawala na watu wakakusanyika juu yake, wakamridhia na akawashinda kwa upanga wake mpaka yeye akawa ndiye khaliyfah, basi ni lazima kumtii na ni haramu kufanya uasi dhidi yake.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya ´Aqiydah ni kuwasikiliza na kuwatii watawala wa waislamu. Hilo ni kwa ajili ya kutendea kazi maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[1]

Baada ya kuamrisha kumtii Yeye na kumtii Mtume Wake ameamrisha kuwatii watawala wa waislamu. Hapo ni pale aliposema:

مِنكُمْ

“… katika nyinyi.”

Bi maana katika waislamu.

Lakini akiwa sio muislamu hakuna utiifu juu yake. Ni sharti awe muislamu. Hapo ndipo itakuwa ni lazima kumtii. Kufanya uasi dhidi yake ni maasi na haramu. Huu ni msingi miongoni mwa misingi ya Uislamu. Umoja wa waislamu na nguvu zao zinapatikana kupitia jambo hilo.

Wakati Maswahabah walipohisi kukaribia kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo wakamuomba awausie akasema:

“Nawausieni juu ya kumcha Allaah, kusikiliza na kutii ijapokuwa mtatawaliwa na mja… “[2]

Kinachozingatiwa si yeye kama yeye. Kinachozingatiwa ni ile nafasi alionayo. Kinachozingatiwa ni ile nafasi alionayo na si yeye kama yeye:

“… ijapokuwa mtatawaliwa na mja. Hakika yule miongoni mwenu atakayeishi kipindi kirefu basi ataona tofauti nyingi.”

Kumtii mtawala ni kinga dhidi ya tofauti. Kwa ajili hii wakati Hudhayfah bin al-Yamaan alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya fitina wakati itapojitokeza akamuuliza: “Unaniamrisha nini nikikutana na jambo hilo?” Akasema: “Kulazimiana na mkusanyiko wa waislamu na kiongozi wao.”[3]

Akamwamrisha Hudhayfah wakati kutapodhihiri fitina alazimiane na mkusanyiko wa waislamu na mtawala wao. Kwa sababu ndio kinga dhidi ya fitina na kinga dhidi ya tofauti:

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚ وَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana baada ya kuwajia hoja za wazi – na hao watapata adhabu kuu.”[4]

Kwa hiyo kutofautiana ni shari na kuafikiana na rehema.

[1] 04:59

[2] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676), Ibn Maajah (42) na Ahmad (04/126 nambari. 17144) kupitia kwa al-´irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh).

[3] al-Bukhaariy (3606) na Muslim (1847) kupitia kwa Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] 03:105

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 127-128
  • Imechapishwa: 31/05/2021