Zakaat-ul-Fitwr ni faradhi iliyofaradhisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindipo Ramadhaan inapokwisha. ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaradhisha kutoa pishi ya tende au pishi ya ngano kuwa ni Zakaatul-Fitwr iliyowajibika kwa waislamu wote; mtumwa, muungwana, mwanamume, mwanamke, mtoto mdogo na mzee na kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali.”[1]
Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.
Chakula kinatakiwa kuwa kile kinacholiwa na watu. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:
“Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulikuwa tukitoa Zakaatul-Fitwr pishi moja ya chakula, pishi ya ngano, pishi ya tende, pishi ya mtindi mkavu au pishi ya zabibu.”[2]
Ameipokea al-Bukhaariy.
Haijuzu kutoa Zakaat-ul-Fitwr pesa, magodoro, nguo, mifugo, samani na venginevyo. Kwa sababu hayo yanaenda kinyume na yale aliyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Yeyote mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, basi kitarudishwa kwake.”[3]
Bi maana atarudishiwa yeye mwenyewe.
Pisi moja ni sawa na gramu 2400 ya ngano zuri. Hiki ndio kipimo cha kinabii cha Zakaat-ul-Fitwr.
Ni wajibu kutoa Zakaat-ul-Ftwr kabla ya kwenda kuswali swalah ya ´Iyd. Bora ni kuitoa siku ya ´Iyd kabla ya swalah ya ´Iyd. Hata hivyo ni sahihi kuitoa siku moja au mbili kabla ya ´Iyd. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefaradhisha Zakaat-ul-Fitwr ili mfungaji atwahirishwe na maneno ya upuuzi na maneno machafu na pia kuwalisha chakula masikini. Yule mwenye kuitoa kabla ya swalah, basi hiyo ni zakaah yenye kukubaliwa, na mwenye kuitoa baada ya swalah, basi hiyo ni swadaqah miongoni mwa swadaqah.”[4]
Ameipokea Abu Daawuud na Ibn Maajah.
Lakini lau hakujua kuwa ni ´Iyd isipokuwa baada ya swalah au wakati wa kuitoa alikuwa mashambani au mahali ambapo hakuna mwenye kuistahiki, ni sahihi akaitoa baada ya swalah ya ´Iyd pale atapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo na Allaah ndiye anajua zaidi.
Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, jamaa zake na Maswahabah zake.
[1] al-Bukhaariy (1503) na Muslim (984).
[2] al-Bukhaariy (1508) na Muslim (985).
[3] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).
[4] Abu Daawuud (1609), Ibn Maajah (1827), ad-Daaraqutwniy (2/138) na al-Haakim (1/409) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1420).
- Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 22-23
- Imechapishwa: 05/06/2017
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket