9 – Shaykh na ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy (Hafidhwahu Allaah)

Amesema (Hafidhwahu Allaah) katika sifa zake juu ya kitabu “Jamaa´ah Waahidah laa Jamaa´aat”:

“Ni wajibu kwa yule anayejua ana uwezo wa kuweza kupambanua baina ya haki na batili, kufanya hivo. Shaykh Rabiy´ ni mmoja katika waliojijaribu wenyewe katika misimamo hii ya mapambano na amefaulu – himdi zote njema ni Zake Allaah… Ninaonelea kuwa Shaykh Rabiy´ amefaulu katika kuweza kuyakosoa makosa haya na kuyaraddi kwa dalili sahihi, fikira za kisawa na usulubu wa kati na kati. Allaah Amjaze kheri na Amlipe kwa wakati na juhudi zake alizotumia. Ninawanasihi vijana wasome kitabu chake ili wasidanganyike na Bid´ah. Ee Allaah, tuoneshe haki kuwa ni haki na Aturuzuku kuweza kuifuata, na Atuoneshe upotevu kuwa ni upotevu na Aturuzuku kuweza kujiepusha nao na usiufanye ukawa ni wenye kututatiza na tukapotea.”[1]

Amesema vilevile katika kanda “Ahkaam-ul-´Ulamaa´ fiy Maqaalaat ´Adnaan ´Ar´uur”:

“Shaykh Rabiy´ anajulikana katika kupigana kwake Jihaad kwa kuidhihirisha Sunnah na kuwaraddi watu wa Bid´ah. Allaah Amjaze kheri.”

Kadhalika aliulizwa swali (Hafidhwahu Allaah):

“Ni yepi maoni yako kwa yule mwenye kumsema vibaya Shaykh Rabiy´ bin Haadiy na Shaykh Faalih al-Harbiy?”

Akajibu:

“Yule mwenye kuwasema vibaya watu hawa ni dalili inayoonesha kuwa ana kitu kisichokuwa kilichojificha na ima ni mtu wa Bid´ah au mwenye kuwasaidia watu wa Bid´ah na anashirikiana nao. Watu hawa ni watu wa Sunnah na hakuna anayewasema vibaya isipokuwa yule ambaye amepewa mtihani au ni mpotevu. Tunamuomba Allaah Atuongoze sisi sote.”

Aliulizwa (Hafidhwahu Allaah) swali lifuatalo:

“Je, Shaykh Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy na ´Adhaan ´Ar´uur wanaweza kuzingatiwa ni wapinzani?”

Akajibu:

“Hapana, hapana. Haiwezekani mchanga ukalinganishwa na dhahabu. Imedhihirika kuwa ´Adhaan ´Ar´uur ni Hizbiy. Anawatetea Hizbiyyuun. Anawasema vibaya Salaf. Anataka kuwajeruhi Salafiyyuun. Anataka kuwaponda Salafiyyuun wakati huohuo anawatetea watu wa Bid´ah. Ama kuhusiana na Shaykh Rabiy´, anajulikana kupambana kwake Jihaad kwa kuidhihirisha Sunnah na kuwaraddi watu wa Bid´ah.”

Amesema pia katika Radd yake kwa Abul-Hasan al-Miswriy:

“Shaykh Rabiy´ ni mtu anayepigana Jihaad kwa ajili ya Allaah. Allaah Amjaze kheri. Natamani na mimi pia lau ningelikuwa napigana vita kama jinsi anavyofanya kwa kueneza Sunnah, kuiponda Bid´ah na watu wake na kutilia umuhimu mkubwa katika Sunnah na kuieneza. Ninamuomba Allaah Amjaze kwa kheri iliokuwa nzuri. Kwa ajili hiyo ndio maana mimi na Ahl-usSunnah wengine wote tunampenda.”

Kadhalika amesema katika Radd ya Shaykh Rabiy´ kwa mpotevu mmoja Raafidhwiy kwa jina la Hasan Farhaan al-Maalikiy:

“Hivyo Shaykh Rabiy´ akakabiliana naye ambaye ana uzowefu wa utata huu kwa muda mrefu kwa kupigana kwake Jihaad katika njia ya Allaah, kuwaponda maadui wa Allaah na kubainisha upotevu wa watu wa Bid´ah hawa ambao wanadai kuwa ni “uongofu”. Kwa ajili hiyo apewe hongera kwa Jihaad aliyosimama nayo kwa manufaa ya Uislamu na kutetea Sunnah Twaharifu. Allaah Amjaze kheri na Ambariki. Ninamuomba Allaah Atupe uthabiti sisi na yeye katika haki.

Amebainisha upotevu wa Sayyid Qutwub, upindaji wa ´Abdur-Rahmaan ´Abdul-Khaaliq na upetukaji mpaka wa Haddaadiyyah. Amekabiliana na Khawaarij wa leo, makundi ya Takfiyr, kwa njia ambayo mkosoaji mwenye uzowefu tu na dereva imara ndiye awezaye kufanya. Amebainisha makosa yao na upotevu. Kisha amekabiliana na Abul-Hasan al-Miswr al-Ma´ribiy na akafichukua urukaji mipaka wake na udanganyifu wake. Mwishoni akabainisha uongo wa al-Maalikiy, hila zake, uongo wake na hadaa zake ambazo kwazo amewatumikia Raafidhwah wenye chuki na Suufiyyah mazanadiki.”

Kisha akasema:

“Allaah Amjaze kheri Shaykh Rabiy´ kwa kheri iliokuwa nzuri, Ambariki na katika ulinganizi na Jihaad yake na Atujaalie sisi na yeye kuwa katika wale wanaotetea Shari´ah yake kwa kiasi cha kila mtu awezavyo.”

Aliulizwa (Hafidhwahu Allaah) swali lifuatalo:

“Muheshimiwa Shaykh Ahmad, ni yepi maoni yako kwa mwenye kusema ´Simtambui si Shaykh Zayd al-Madkhaliy wala Rabiy´ al-Madkhaliy kuwa ni wanachuoni na sitambui chochote katika elimu kutoka kwao. Ninayemtambua tu ni Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz`? Unasemaje juu ya hili?”

Akajibu (Hafidhwahu Allaah) ifuatavyo:

“Tunamuomba Allaah Amuongoze. Shaykh Rabiy´ al-Madkhaiy na Shaykh Zayd al-Madkhaliy wote wawili ni katika wanachuoni wa Salafiyyah na wanasihiaji. Ni wajibu kwake atambue na ajue hilo. Asiwaseme vibaya kwa kuwa ina maana ni kuzisema vibaya Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo wamebeba. Hata hivyo hatusemi kuwa wamekingwa na makosa, lakini tunasema kuwa mfumo wao ni wa Salafiyyah. Ni wajibu kwa wanafunzi kusoma vitabu vyao na waitambue haki ima kupitia kwao au vitabu vya wengine. Tahadharini na vitabu vya Hizbiyyuun. Ikiwa unataka kuchukua hili moja kwa moja kutoka kwa Shaykh Ibn Baaz, basi unaweza daima kumwandikia moja kwa moja na kumuuliza maoni yako juu ya fulani na fulani. Hivyo ikiwa atasema kuwa ni waharibifu, Hizbiyyuun na hakuna kheri yoyote kwa watu hawa, kubali hilo na uendelee kubaki katika msimamo wako huo. Hata hivyo mimi nina uhakika ya kwamba atawasifu.”

Aliulizwa (Hafidhwahu Allaah) swali lifuatalo:

“Ni kweli kwamba Shaykh Rabiy´ ni mmoja katika wanafunzi zako?”

Akajibu:

“Shaykh Rabiy´ alisoma kwenye Ma´had na mimi ni katika waliomsomesha kwenye Ma´had. Lakini, Shaykh Rabiy´ ni bora kuliko mimi. Anapigana Jihaad katika kuihuisha Sunnah, kuziua Bid´ah na kuwaraddi watu wa Bid´ah. Amejitaalumisha mwenyewe katika jambo hili. Tunamuomba Allaah Atuwafikishe sisi sote kwa yale Anayoyapenda na kuyaridhia.”

Katika muhadhara huohuo amesema:

“Anayemsema vibaya Shaykh Rabiy´ na Shaykh Faalih al-Harbiy anachukia Salafiyyah, kwa sababu watu hawa ndio viongozi wa Salafiyyah.”[2]

Amesema (Hafidhwahu Allaah) kuhusu Radd yake dhidi ya Faalih al-Harbiy akimsapoti Shaykh Rabiy´:

“Tunamjua Shaykh Rabiy´ tangu miaka kadhaa ya nyuma mwenye uzowefu wa kuinusuru Sunnah, akiitetea na akitetea utukufu wake. Ametunga tungo, ameandika makala mbalimbali na  ameraddi mambo yanayoenda kinyume. Tunamzingatia kuwa amefanya hivo kwa ajili ya kuinusuru dini na kuwafichua wale wote wenye kwenda kinyume. Ruduud zake hizo na vitabu vyake ni vyenye kushuhudia juu ya hilo.

Huenda wanafunzi wengi hawajui yale tunayoyajua. Yeye ndiye kamraddi Sayyib Qutwub na akabainisha makosa yake. Yeye ndiye kamraddi ´Abdur-Rahmaan ´Abdul-Khaaliq. Yeye ndiye kamraddi Mahmuud al-Haddaad na akabainisha kuvuka kwake mpaka na kupetuka kwake. Yeye ndiye kamraddi ´Adnaan ´Ar´uur, [Salmaan] al-´Awdah, [Safar] al-Hawaaliy, Ma´ribiy, Hasan al-Maalikiy na wengineo. Kisha anakuja mtu mwenye malengo fulani na kusema: “Shaykh Rabiy´ ni Mumayyi´, neno lililo na maana – kutokana na tunavyojua – kwamba hawasemi Ahl-ul-Bid´ah waziwazi juu ya Bid´ah zao na wala hawahukumu kwazo. Kufanya hivi ni kumsemea uongo, kumfanyia uadui na kuangusha juhudi zake. Ikiwa mtu atasema kuwa hii leo hakuna mtu anayewakataa Ahl-ul-Bid´ah, kuwapiga vita na kuyajadili makosa yao kama anavofanya Shaykh Rabiy´ (Wafaqahu Allaah) basi amesema kweli. Tunaamini kuwa anafanya hivo kwa kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall) na hali ya kutekeleza faradhi ambayo Allaah amewafaradhishia wanachuoni.  Kufanya kitu kama hicho kinahitajia juhudi  na kutenga wakati wa kutosha. Ikhlaasw alionayo kwa Allaah (´Azza wa Jall) inamfanya kufanya anayoyafanya na wakati huohuo akili yake ni yenye kutulizana, moyo mtulivu, mwenye yakini na thawabu za Allaah na mwenye subira juu ya yale maudhi, uadui na vitimbi yanayomkabili katika njia hiyo. Haya ndio tunayoamini juu yake na tunataraji hali ni hiyo. Je, hivi kweli haoni haya yule ambaye anamtuhumu Tamayyu´? Mtu akimuuliza kama yeye amefanya nusu ya yale yaliyofanywa na Shaykh Rabiy´, robo yake au thumuni yake, jibu lake litakuwa lipi?

Shaykh Rabiy´ ana shauku kubwa kwa yale anayoona kuwa na manufaa juu ya mfumo wa Salaf. Tunaamini kuwa ana akili yenye nguvu na kuyapa kipaumbele manufaa jambo ambalo wakati mwingine linamfanya kutokana na manufaa ya Da´wah kutotoa baadhi ya mambo na kuyamaliza kwa njia maalum. Matokeo yake baadhi ya watu wakadhani kuwa amefanya hivo kwa sababu ya kutaka kuwapaka mafuta baadhi ya watu na kuwabagua wengine. Yule ambaye anayakadiria mambo ipasavyo hatakiwi kuharakisha dhana kama hizi na afunge safari kwenda kwa Shaykh na azungumze naye kwa siri. Si mtu mwenye kukataa – Allaah akitaka – kwa jambo lenye manufaa. Hayo ndio yenye kunibainikia kuhusu hali yake – Allaah amuhifadhi – na Allaah ni mwenye kuzitambua nia zote.”

Shaykh Ahmad an-Najmiy (Hafidhwahu Allaah) ni katika waalimu wa Shaykh Rabiy´. Alimsomesha kwenye Chuo Kikuu cha elimu Swaamitwah kabla ya Shaykh Rabiy´ kukubaliwa kwenye Chuo Kikuu cha Kiislamu. Shaykh Ahmad alimpa cheti cha Hadiyth ambapo alimpa rukhusa na idhini ya kufundisha Hadiyth.

[1] Tazama dibaji ya kitabu cha Shaykh Rabiy´ ”an-Naswr al-´Aziyz”

[2] Muhadhara Juddah, 1423/5/25.

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.rabee.net/ar/sharticles.php?cat=12&id=57
  • Imechapishwa: 03/12/2019