Wanaowafuatia Maswahabah katika fadhilah, heshima na nafasi ni viongozi wa waongofu katika Taabi´uun, waliokuja baada yao katika karne bora na pia waliokuja baada yao miongoni mwa wale waliowafuata Maswahabah kwa wema. Amesema (Ta´ala):

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ

“Wale waliotangulia wa mwanzo [katika Uislamu] miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye.”[1]

Kwa hivyo haijuzu kuwaponda na kuwatukana. Kwa sababu wao ndio viongozi wa uongofu. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”[2]

Mshereheshaji wa at-Twahaawiyyah amesema:

“Ni lazima kwa kila muislamu, baada ya kumpenda Allaah na Mtume Wake, awapende waumini kama ilivyotaja Qur-aan na khaswakhaswa wale ambao ndio warithi wa Mitume ambao Allaah amewafanya katika manzilah ya nyota; watu wanaongozwa kupitia wao katika viza vya nchikavu na bahari. Waislamu wameafikiana juu ya kuongoza kwao na maarifa yao.”[3]

Wao ndio wanashika nafasi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Ummah wake na wanazihuisha zile Sunnah zake zilizokufa. Qur-aan imesimama na kutamka kupitia wao na kwa ajili yao. Wote wameafikiana maafikiano yenye yakini juu ya ulazima wa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini mmoja wao akisema maneno inayokwenda kinyume na Hadiyth Swahiyh basi ni lazima awe na udhuru kwa kule kuiacha kwake. Nyudhuru zote zimegawanyika aina tatu:

Ya kwanza: Haonelei kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema hivo.

Ya  pili: Haonelei kuwa amekusudia masuala hayo kwa maneno hayo.

Ya tatu: Anaonelea kuwa hukumu imefutwa.

Wana fadhilah na neema juu yetu kwa kutangulia, kutufikishia yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutuwekea wazi yale yenye kujificha kwetu – Allaah amewawia radhi nao wamemuia radhi:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[4]

Kutia dosari nafasi ya wanachuoni kwa sababu ya kupatikana kosa la ki-Ijtihaad kutoka kwa baadhi yao ni mwenendo wa wazushi na ni mbinu za maadui wa Ummah. Lengo ni kutaka kuitia mashaka dini ya Uislamu, kueneza uadui kati ya waislamu, kutenganisha waliokuja nyuma kutokamana na watangu wao na kuleta mpasuko kati ya vijana na wanachuoni – kama hali ilivyo hii leo. Wazinduke juu ya hayo baadhi ya wanafunzi wenye kuanza ambao wanapoteza nafasi ya Fuqahaa´ na kutokamana na nafasi ya uelewa wa Kiislamu. Isitoshe wanapuuza kuisoma, kunufaika na ile haki na usawa unaopatikana ndani yake, wamejitosheleza kutokamana na uelewa wao na hawawaheshimu wanachuoni wao. Asidanganyike na madai yenye kupotosha na yenye malengo yasiyokuwa mazuri.

[1] 09:100

[2] 04:115

[3] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 555.

[4] 59:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 174-176
  • Imechapishwa: 25/06/2020