Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye mioyo na ndimi ziliosalimika kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama Allaah alivowasifu juu ya hilo pale aliposema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

Pia kwa sababu ya kumtii Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake lau mmoja wenu atatoa dhahabu kiasi cha mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vilivyojazwa na mikono vya mmoja wao wala nusu yake.”[2]

Wanajitenga mbali na mwenendo wa Raafidhwah na Khawaarij wanaowatukana Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), kuwachukia, kuzipinga fadhilah zao na kuwakufurisha wengi wao.

Ahl-us-Sunnah wanazikubali zile fadhilah zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah na wanaamini kuwa wao ndio karne bora. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wabora wenu ni wa karne yangu… “[3]

Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotaja kwamba Ummah wake utafarikiana katika mapote sabini na tatu na kwamba yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu na akaulizwa kuhusu kundi hilo ambapo akasema:

“Ni wale wataokuwa juu ya yale niliyomo hii leo na Maswahabah wangu.”[4]

Abu Zur´ah, ambaye ni mtukufu zaidi wa waalimu wa Imaam Muslim, amesema:

“Ukimuona mtu anamtukana mmoja katika Maswahabah basi utambue kuwa ni zandiki. Hivo ni kwa sababu Qur-aan ni haki, Mtume ni haki na aliyokuja nayo ni haki. Hakuna waliotufikisha yote hayo isipokuwa ni Maswahabah. Mwenye kuwatukana malengo yake ni kuijeruhi Qur-aan na Sunnah. Hivyo yeye ndiye anastahiki zaidi kujeruhiwa. Yeye ndiye ana hakii zaidi ya kuhukumiwa uzandiki na upotevu.”[5]

´Allaamah Ibn Hamdaan amesema mwishoni mwa “al-Mubtadi-iyn”:

“Mwenye kumtukana mmoja katika Maswahabah hali ya kulihalalisha hilo amekufuru. Asipolihalalisha hilo basi amefanya ufuska. Vilevile imepokelewa kutoka kwake kwamba anakufuru moja kwa moja. Na yule mwenye kuwatukana katika dini yao au akawakafirisha amekufuru.”[6]

[1] 59:10

[2] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

[3] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (6422).

[4] at-Tirmidhiy (2646).

[5] as-Swawaa´iq al-Mursalah (02/608).

[6] Sharh ´Aqiydah as-Safaariyniyyah (02/388-389).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 173-174
  • Imechapishwa: 25/06/2020