Hivi ndivo ulivyo uombezi uliothibiti kwa sharti zake. Ni sampuli mbalimbali. Baadhi ya sampuli ni maalum zinamuhusu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na aina zingine anashirikiana yeye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mitume wengine, Malaika, waja wema na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe – wote hawa watafanya uombezi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kama tulivyosema kuna aina mbalimbali ya uombezi ambao ni maalum zinamuhusu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), nao ni:

1 – Atawaombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) watu wataokuwa wamekusanyika kiwanjani siku ya Qiyaamah. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ndiye bwana wa watu siku ya Qiyaamah? Mnajua ni kwa nini? Siku ya Qiyaamah Allaah atawakusanya watu wote sehemu moja. Watamsikia mwitaji, macho yao yamekodolewa na jua litasogezwa karibu nao. Baadhi ya watu watasema: ”Hivi hamuoni yale mliyomo? Hivi hamtazami ni nani awezaye kuwaombea mbele ya Mola wenu?” Baadhi ya watu watasema: ”Baba yenu Aadam.” Waende kwa Aadam na waseme: “Ee Aadam! Hakika wewe ndiye baba wa watu. Allaah amekuumba kwa mkono Wake, akakupulizia roho Yake na akawaamrisha Malaika kukusujudia. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Aadam atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Alinikataza kula katika mti ambapo nikamuasi. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Nuuh.” Waende kwa Nuuh na kusema: “Ee Nuuh! Wewe ndiye Mtume wa kwanza kutumilizwa ardhini. Allaah amesema kuwa wewe ni mja mwenye kushukuru. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Nuuh atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Nilikuwa na haki ya du´aa yenye kuitikiwa na nikaiomba dhidi ya watu wangu. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Ibraahiym.” Waende kwa Ibraahiym na kusema: “Ee Ibraahiym! Wewe ni kipenzi mwandani kabisa wa Allaah na Mtume Wake ardhini. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Ibraahiym atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake.” Atataja kusema kwake uongo mara tatu kisha atasema: “Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muusa.” Waende kwa Muusa na kusema: “Ee Muusa! Wewe ni Mtume wa Allaah! Allaah amekuteua kutokamana na watu wengine wote kwa ujumbe na maneno Yake. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Muusa atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Niliua nafsi bila idhini. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa ´Iysaa.” Waende kwa ´Iysaa na kusema: “Ee ´Iysaa! Wewe ni Mtume wa Allaah. Uliwazungumzisha watu katika hali ya uchanga. Wewe ni neno Lake alilolirusha kwa Maryam na roho inayotokamana Naye. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” ´Iysaa atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muhammad.” Waende kwa Muhammad na kusema: “Ee Muhammad! Wewe ni Mtume wa Allaah na Nabii wa mwisho. Allaah amekusamehe dhambi zako zote. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Nitaondoka mpaka nitakapofika chini ya ´Arshi ambapo nitasujudu mbele ya Mola wangu. Kisha Allaah ataniidhinisha kumhimidi kwa njia ambayo hajapatapo kuhimidiwa na mwingine yeyote. Ataambiwa: “Ee Muhammad! Inua kichwa chako. Uliza utapewa, omba utapokelewa uombezi wako.” Nitainua kichwa changu na kusema: “Ee Allaah! Ummah wangu! Ummah wangu!” Kutasemwa: “Ee Muhammad! Wale ambao katika Ummah wako ambao hawatofanyiwa hesabu waingize Peponi kupitia milango yake ya kulia. Milango mingine yote ya Peponi watashirikiana na wengineo.” Naapa kwa Yule ambaye mkononi Mwake iko roho yangu umbali kati ya milango miwili ya Pepo ni kama umbali kati ya Makkah na Hajar, au ni kama umbali kati ya makkah na Busraa.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataomba baada ya kuomba du´aa na kupewa idhini na Mola wake. Si kwamba ataombea moja kwa moja; bali atasujudu, kuomba du´aa, kumsifu Allaah na kutawasali Kwake kwa majina na sifa Zake.  Baada ya hapo ndio atapewa idhini ya kuombea. Kisha aombee kuhukumiwe kati ya viumbe ambapo Allaah akubali uombezi wake na ndipo Allaah atakuja ili hukumumu kati ya waja Wake. Allaah (Subhaanah) amesema:

كَلَّا إِذَا دُكَّتِ الْأَرْضُ دَكًّا دَكًّا وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

”Sivyo hivyo! [Kumbukeni pale] ardhi itakapovunjwavunjwa. Na Atakapokuja Mola wako, na Malaika safu kwa safu.”[2]

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ وَقُضِيَ الْأَمْرُ

“Je, wanangojea [nini] isipokuwa Allaah Awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika na itolewe hukumu?”[3]

Uombezi huu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni nafasi tukufu ambayo Allaah amemtukuza kwayo. Ni cheo chenye kusifiwa ambacho Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema juu yake:

عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا

”Hapana shaka Mola wako atakuinua cheo kinachosifika.”[4]

Kwa sababu atasifiwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na viumbe wote juu yake. Hapo ndipo kutaonekana ubora wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika nafasi hii tukufu.

[1] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (194).

[2] 89:21-22

[3] 2:210

[4] 17:79

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 96-100
  • Imechapishwa: 25/01/2023