87. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya kujitokeza kwa ad-Dajjaal

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Jihaad ni yenye kuendelea tangu hapo Allaah alipomtumiliza Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka pale mtu wa mwisho wa Ummah huu atakapomuua ad-Dajjaal. Haibatilishwi kwa dhuluma ya mwenye kudhulumu wala uadilifu wa mwenye kufanya uadilifu.

MAELEZO

ad-Dajjaal ni al-Masiyh ad-Dajjaal mwongo. Ameitwa ad-Dajjaal kwa sababu ya uongo wake mwingi na kutokana na ile fitina kubwa alionayo. Kila Nabii aliutahadharisha Ummah wake kutokana na al-Masiyh ad-Dajjaal. Ambaye alifanya hivo sana ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye aliye karibu zaidi na kujitokeza kwake. Atajitokeza katika zama za mwisho. Atajitokeza kwa mayahudi. Kukusanyika kwa mayahudi hii leo huko Palestina ni utangulizi wa kujitokeza kwa ad-Dajjaal. Kwa sababu atajitokeza kwa mayahudi – Allaah awakebehi.

Kutatokea kwake fitina kubwa na itazunguka katika miji mbalimbali. Hakuna mji wowote isipokuwa ataingia isipokuwa Makkah na Madiynah. Hatoingia ndani yake. Lakini waovu waliyoko Makkah na Madiynah watatoka kumfuata. Hawatobaki ndani yake isipokuwa waumini tu. Kwa sababu ad-Dajjaal akija Madiynah itatetemeka na atoke ndani yake kila mnafiki na hawatobaki ndani yake isipokuwa waumini wa kweli. Kisha atateremka ´Iysaa bin Maryam, ambaye ni al-Masiyh wa uongofu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atateremka kutoka mbinguni kisha atamtafuta ad-Dajjaal amuue katika mlango wa Ludd huko Palestina. Atamuua na Allaah aunusuru Uislamu na waislamu. al-Masiyh bin Maryam atahukumu kwa Uislamu ambayo ni dini ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uislamu utakuwa na nguvu katika kipindi chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati watapokuwa katika hali hiyo ndipo atajitokeza Ya´juuj na Ma´juuj waliotajwa na Allaah (´Azza wa Jall). Allaah atamwamrisha ´Iysaa akimbie akawahifadhi waislamu katika mlima wa Twuur na aseme:

“Mimi nimewatoa waja Wangu hakuna yeyote ana nguvu za kupigana na wao. Hivyo wahifadhi waja Wangu katika [mlima wa] Twuur.”

Waeneze ufisadi juu ya ardhi na wawachinje baadhi ya waislamu. Kisha Allaah awateremshie maradhi wafe. Allaah awapumzishe waislamu kutokamana nao. Hiki ndio kisa cha kujitokeza kwa ad-Dajjaal kwa ufupi. Sisi tunaamini kujitokeza kwa al-Masiyh ad-Dajjaal.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 26/05/2021