88. Dalili juu ya kuteremka kwa ´Iysaa katika zama za mwisho

Vipo vitabu vya wajinga wanaosema kuwa ad-Dajjaal hayupo. Wanasema kuwa hiyo ni ibara ya uongo mwingi katika zama za mwisho na kwamba hakuna jambo la kuteremka kwa ´Iysaa. Wanasema kuwa hiyo ni ibara ya kudhihiri kwa haki. Huku ni kupinga jambo lililopokelewa kwa wingi katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali Qur-aan imefahamisha juu ya kuteremka kwa ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ

“Hakuna yeyote katika Ahl-ul-Kitaab isipokuwa atamwamini kabla ya kufa kwake.”

Hii ni dalili juu ya kwamba atateremka katika zama za mwisho. Mayahudi waliomkufuru hapo mwanzo watamwamini:

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا

“Hakuna yeyote katika Ahl-ul-Kitaab isipokuwa atamwamini kabla ya kufa kwake na siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao.”[1]

Katika Aayah nyingine amesema juu ya ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِّلسَّاعَةِ

“Hakika yeye ni alama ya Saa.”[2]

Bi maana kuteremka kwake katika zama za mwisho ni alama za kukaribia kwa Qiyaamah. Kuna kisomo kinasomwa:

وَإِنَّهُ لَعِلَمٌ لِلسَّاعَةِ

“Hakika yeye ni alama ya Saa.“[3]

Kuteremka kwa ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka mbinguni ni alama juu ya kukaribia kwa Qiyaamah. Ni miongoni mwa alama na ishara za Qiyaamah.

[1] 04:159

[2] 43:61

[3] Kimesomwa na Ibn ´Abbaas, Qataadah na adh-Dhwahhaak. Tazama ”Tafsiyr-ut-Twabariy” (25/90-91).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 125-126
  • Imechapishwa: 26/05/2021