Mayahudi walifanya njama dhidi ya Uislamu na watu wake. Wakaingiza vitimbi vichafu kwa kudhihirisha Uislamu kwa uongo na uzushi. Naye si mwengine ni ´Abdullaah bin Sabaa´ ambaye alikuwa ni myahudi wa Yemen. Myahudi huyu akaanza propaganga zake za chuki na sumu dhidi ya khaliyfah wa tatu miongoni mwa makhaliyfah waongofu; ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) na akileta tuhuma mbalimbali dhidi yake. Wakamzunguka wale waliohadaika naye kutokana na mtazamo wao mfupi, imani yao dhaifu na kupenda fitina. Njama hizo zikamalizikia kuuawa kwa khaliyfah huyu mwongofu ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) akiwa ni mwenye kudhulumiwa. Kutokana na athari ya kuuliwa kwake kukatokea tofauti kati ya waislamu na fitina ikapamba moto kwa sababu ya uchochezi kutoka kwa myahudi huyu na wafuasi zake na kukatokea mauaji kati ya Maswahabah kutokana na Ijtihaad zao. Mshereheshaji wa at-Twahaawiyyah amesema:

“Msingi wa madhehebu ya Raafidhwah yamezuliwa na mnafiki na zandiki. Lengo lake ilikuwa kuitokomeza dini ya Uislamu na kumponda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama walivosema wanachuoni. ´Abdullaah bin Sabaa´ wakati alipodhihirisha Uislamu alicholenga ni kuiharibu dini ya Uislamu kwa vitimbi na uchafu wake – kama alivofanya Paulo juu ya dini ya ukristo – akadhihirisha kuipa nyongo dunia, kisha akadhihirisha kuamrisha mema na kukataza maovu mpaka akafanikiwa juu ya fitina kwa ´Uthmaan na kuuliwa kwake. Halafu alipofika Kuufah akadhihirisha kuchupa mpaka kwa ´Aliy na kumnusuru ili kupitia njia hiyo aweze kufanikiwa malengo yake. Hayo yakamfikia ´Aliy na akamtafuta kumuua. Ndipo akakimbia kwenda Qarqays. Khabari zake zinatambulika katika historia.”[1]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wakati alipouawa Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) mioyo ikatofautiana, majanga yakawa makubwa, shari zikadhihiri, wema wakadhalilika, wakajaribu kuingia ndani ya fitina wale waliokuwa wameshindwa kufanya hivo, wakashindwa kufanya kheri na wema wale waliokuwa wanapenda kutekeleza mambo hayo. Baadaye wakampa kiapo cha usikivu kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) – na yeye wakati huo ndiye alikuwa na haki zaidi ya kuongoza na ndiye mbora zaidi aliyekuwa amebaki. Lakini hata hivyo mioyo ilikuwa imetofautiana na moto wa fitina ulikuwa tayari umeshawaka. Matokeo yake umoja haukuungana na khaliyfah na wabora wa Ummah hawakufanikiwa kwa kila kheri waliyokuwa wanaitaka. Baadhi ya watu wakaingia ndani ya tofauti na fitina na kukatokea yaliyotokea.”[2]

Vilevile amesema akibainisha udhuru wa wale Maswahabah waliopigana katika mapigano ya ´Aliy na Mu´aawiyah:

“Mu´aawiyah hakudai uongozi, hakupewa kiapo cha usikivu wakati alipouliwa ´Uthmaan, hakuuliwa kujengea kwamba ni kiongozi au kwamba yeye ndiye anastahiki uongozi. Mu´aawiyah alikuwa akilikubali hilo kwa yule mwenye kumuuliza jambo hilo. Bali Mu´aawiyah na wenzake walikuwa wanaona waanze kwanza [kulipiza kisasi] juu ya wale waliokuwa upande wa ´Aliy na wenzake. Upande wa pili ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na wenzake wao wakawa wanaona kuwa ni lazima kwanza watiiwe na kupewa kiapo cha usikivu na waislamu wawe na khaliyfah mmoja peke yake, wakaona kuwa wenzao wametoka nje ya utiifu, wamejizuia kutokamana na wajibu huu na wao ndio wenye nguvu, ndipo wakaona wawapige vita mpaka watimize wajibu huu na kupatikane utiifu na umoja. Upande wa kwanza walikuwa wanaona kuwa jambo hilo sio la lazima kwao na kwamba wakipigwa vita kutokana na hilo basi watakuwa ni wenye kudhulumiwa kwa sababu walikuwa wanaona kuwa ´Uthmaan ameuliwa kwa kudhulumiwa kwa maafikiano ya waislamu na waliomuua walikuwa katika jeshi la ´Aliy na walikuwa ni wenye kuwashinda nguvu. Kwa hivyo walikuwa wanaona wakikataliwa watakuwa wamewadhulumu na wamewafanyia uadui. ´Aliy hakuweza kuwazuia kama alivyoshindwa kuwazuia kutokamana na ´Uthmaan. Alichokuwa anaona kwamba ni lazima kwao kumpa kiapo cha usikivu kiongozi ambaye anaweza kuwafanyia haki na kuitekeleza kwao kwa uadilifu.”[3]

[1] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 554.

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (25/304-305).

[3] Majmuu´-ul-Fataawaa (35/72-73).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 168-169
  • Imechapishwa: 23/06/2020