85. Sura ya tano: Fadhilah za Maswahabah na ambayo ni lazima kuamini juu yao na madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu yaliyopitika kati yao

Swahabah ni nani na ni yepi ambayo ni lazima kuamini juu yao?

Maswahabah ni wingi wa Swahabah. Swahabah ni yule aliyekutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamwamini na akafa juu ya hali hiyo.

Yanayopasa kuamini juu yao ni kwamba wao ndio bora katika Ummah na karne bora kwa sababu ya kutangulia na kusuhubiana kwao na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kupambana bega kwa bega pamoja naye na kufikisha Shari´ah kwa waliokuja baada yao. Allaah amewasifu katika Kitabu Chake kitukufu pale (Ta´ala) aliposema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ

“Wale waliotangulia wa mwanzo [katika Uislamu] katika Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye.”[1]

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖتَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu hali ya kuwa ni wenye kutafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huo ni mfano wao katika Tawraat na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima ili liwaghadhibishe makafiri. Allaah amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema katika aina yao msamaha na ujira mkubwa.”[2]

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Wapatiwe pia mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao wanatafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli. Na wale waliokuwa na makazi [Madiynah] na wakawa na imani kabla yao wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawahisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa [Muhaajiruun] na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe ni wahitaji. Na yeyote anayeepushwa na uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.”[3]

Katika Aayah hizi Allaah (Subhaanah) amewasifu Muhaajiruun na Answaar, akawasifu kutangulia katika mambo ya kheri, akaelezea kwamba amewaridhia na akawaahidi mabustani ya Pepo, akawasifu kwamba ni wenye kuhurumiana kati yao na ni washupavu mbele ya makafiri, akawasifu kwamba ni wenye kurukuu na kusujudu kwa wingi, wenye mioyo mizuri, kwamba wanatambulika kwa alama ya utiifu na imani, kwamba Allaah amewachagua kusuhubiana na Mtume Wake ili wawatie chuki maadui zake makafiri kama alivowasifu Muhaajiruun kuiacha miji na mali zao kwa ajili ya Allaah na kwa ajili ya kuinusuru dini yao na vilevile kutafuta fadhilah na radhi Zake, kwamba ni wakweli katika hilo, akawasifu Answaar kwamba ni watu wa makazi ya kuhajiri na watu wa nusura na wenye imani ya kweli, akawasifu kuwapenda ndugu zao Muhaajiruun, kuwapendelea mema kabla ya nafsi zao, kuwapa nafasi na kusalimika kwao kutokamana na ubakhili – na ndio maana wakafaulu. Hizi ni baadhi ya fadhilah zao za jumla. Zipo fadhilah zao maalum na ngazi ambazo wamefadhilika kwazo wao kwa wao (Radhiya Allaahu ´anhum). Hayo ni kwa kutegemea kutangulia kwao katika Uislamu, Jihaad na kuhajiri.

Mbora katika wale makhaliyfah wane ni Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy. Halafu wanafuatia wale kumi waliobashiriwa Pepo ambao wanaanza hawa wanne kisha anafuatia Twalhah, az-Zubayr, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah, Sa´d bin Abiy Waqqaas na Sa´iyd bin Zayd. Muhaajiruun wanawashinda fadhilah Answaar, waliopigana vita vya Badr  na waliokula kiapo cha usikivu chini ya mti. Ambaye amesilimu kabla ya kufunguliwa mji wa Makkah na akapambana anamshinda fadhilah ambaye amesilimu baada ya kufunguliwa mji wa Makkah.

[1] 09:100

[2] 48:29

[3] 59:08-09

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 166-168
  • Imechapishwa: 23/06/2020