Madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya tofauti na fitina ya vita vilivyotokea kati ya Maswahabah yanafupilizwa katika mambo mawili:

1- Hawazungumzii yaliyopitika kati ya Maswahabah na wanajizuia kuyafanyia utafiti. Kwa sababu njia salama ni kunyamazia mfano wa hayo na wanasema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

2- Majibu juu ya mapokezi yaliyopokelewa kuhusu mabaya yao. Hayo yanajibiwa kwa njia zifuatazo:

Ya kwanza: Katika mapokezi hayo yako ambayo ni ya uongo yamezuliwa na maadui wao ili kuichafua sura yao.

Ya pili: Katika mapokezi hayo yako ambayo yamezidishwa, kupunguzwa ndani yake, kubadilishwa kutoka katika sura yake sahihi na yakaingizwa ndani yake uongo. Kwa msemo mwingine mapokezi hayo yamepotoshwa na ni yenye kupuuzwa.

Ya tatu: Yaliyosihi katika mapokezi hayo – nayo ni machache – ni wenye kupewa udhuru. Kwa sababu wao ima ni wenye kufanya Ijtihaad wakapatia au ni wenye kufanya Ijtihaad wakakosea. Kwa hiyo yanaingia katika mambo ya Ijtihaad ambayo akipatia yule mwenye kufanya Ijtihaad, anapata ujira mara mbili, na akikosea, anapata ujira mara moja na kosa lake linasamehewa. Hayo ni kutokana na Hadiyth ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakimu akijitahidi akapatia, basi anapata ujira mara mbili, na akijitahidi akakosea, basi anapata ujira mara moja.”[2]

Ya nne: Wao ni watu wa kawaida ambao mmojammoja anapitikiwa na makosa. Kwa msemo mwingine wao hawakulindwa na madhambi kwa nisba ya mmojammoja. Lakini pamoja na hivyo kuna mengi mno yenye kufuta yale yale yenye kutokea katika wao ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

1- Kuna uwezekano mtu huyo ametubia kutokamana na hayo. Tawbah inafuta makosa, vovyote yatavyokuwa, kama zilivyothibitisha dalili.

2- Wana utanguliaji na fadhilah ambayo yanawajibisha yale yenye kutoka kwao yakithibiti kweli. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ

“Hakika mema yanaondosha maovu.”[3]

Wana usuhuba na kupambana Jihaad bega kwa bega pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mambo ambayo yanafunika kosa mojamoja.

3- Wanalipwa kwa mema mara zaidi kuliko wanavyolipwa wengine. Hakuna yeyote anayelingana nao katika fadhilah. Imethibiti kwa maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba wao ni karne bora, kwamba Mudd inayotolewa swadaqah na mmoja wao ni bora kuliko mlima wa dhahabu unaotolewa swadaqah na asiyekuwa wao – Allaah amewawia radhi nao wamemuia radhi.

 Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wote wakiwemo maimamu wa dini hawaamini kwamba kuna Swahabah yeyote aliyekingwa na kukosea, nduguzo, wale waliotangulia wala wengineo. Bali kuna uwezekano kutokea kwa madhambi katika wao. Allaah (Ta´ala) amewasamehe kwa kutubia na pia kuwanyanyua kwayo daraja na anawasamehe kwa jema lenye kufuta au kwa sababu nyenginezo. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِي جَاءَ بِالصِّدْقِ وَصَدَّقَ بِهِ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ لِيُكَفِّرَ اللَّـهُ عَنْهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي عَمِلُوا وَيَجْزِيَهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Na yule aliyekuja na ukweli na wakausadikisha, basi hao ndio wenye kumcha Allaah. Watapata yale wayatakayo kwa Mola wao. Hayo ndio malipo ya wafanyao wema; ili Allaah awafutie ukomo wa uovu walioufanya na awalipe ujira wao kwa ukomo wa wema ambao walikuwa wakiutenda.”[4]

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَبَلَغَ أَرْبَعِينَ سَنَةً قَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَصْلِحْ لِي فِي ذُرِّيَّتِي ۖ إِنِّي تُبْتُ إِلَيْكَ وَإِنِّي مِنَ الْمُسْلِمِينَ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ نَتَقَبَّلُ عَنْهُمْ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَنَتَجَاوَزُ عَن سَيِّئَاتِهِمْ فِي أَصْحَابِ الْجَنَّةِ

”Mpaka anapofikia umri wake wa kupevuka na akafikia miaka arobaini husema: “Mola wangu! Nipe ilhamu kuweza kushukuru neema Zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu na nipate kutenda mema utakayoridhia na nitengenezee katika kizazi changu. Kwani hakika mimi nimetubu Kwako na hakika mimi ni katika waislamu. Hao ndio wale ambao Tunawakubalia mazuri zaidi ya yale waliyoyatenda na tunayasamehe makosa yao, watakuwa miongoni mwa watu wa Peponi.”[5]

Maadui wa Allaah wametumia fursa ya yale yaliyopitika kati ya Maswahabah kwenye kipindi cha fitina katika tofauti na mapigano kuwa ndio sababu ya kuwaponda na kudhoofisha hadhi yao. Kupitia mbinu hizi chafu wamepita juu yake baadhi ya waandishi wa kisasa ambao wanayapaparikia wasiyoyajua na matokeo yake wakajifanya wao wenyewe ndio waamuzi kati ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); baadhi wanawafanya kupatia na baadhi ya wengine wanawafanya kukosea bila dalili. Bali wanafanya hivo kwa ujinga na kufuata matamanio. Wanayarudiliarudilia yale yanayosemwa na watu wenye malengo fulani, wenye chuki miongoni mwa wale makafiri na vifaranga vyao mpaka wamewatia mashaka baadhi ya wale waislamu ambao ndio bado wanachipuka – miongoni mwa wale ambao elimu ni chache – juu ya historia yao tukufu na wema wao waliotangulia ambao ndio karne bora. Malengo yao mwishoni ni kufikia kuutukana Uislamu, kufarikisha umoja wa waislamu na kupandikiza chuki mioyoni mwa wale walioko mwishoni mwa Ummah huu badala ya kuwaiga as-Salaf as-Swaalih na kutendea kazi maneno (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”

[1] 59:10

[2] al-Bukhaariy (7352) na Muslim (4462).

[3] 11:114

[4] 39:32-35

[5] 46:15-16 Majmuu´-ul-Fataawaa (35/29-30).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 170-172
  • Imechapishwa: 23/06/2020