Kuhusu uombezi mbele ya Allaah sio kama uombezi kati ya viumbe. Uombezi mbele ya Allaah ni Allaah kuwakirimu baadhi ya waja Wake kuwaombea baadhi ya waislamu wanaostahiki kuadhibiwa kutokana na madhambi yao makubwa waliyoyafanya au ambao wameingia Motoni. Hivyo mwombezi amuombee mbele ya Allaah amsamehe na wala asimuadhibu kwa sababu alikuwa muumini na akimwabudu Allaah peke yake. Huu ndio uombezi kwa watenda madhambi makubwa. Hata hivyo kuombea mbele ya Allaah kunashurutisha sharti mbili:

1 – Ni lazima hayo yafanyike kwa idhini ya Allaah. Hakuna yeyote awezaye kuombea mbele ya Allaah isipokuwa baada ya kupewa idhini. Yeye ndiye ambaye anampa idhini mwombeaji aombe. Hakuna yeyote ambaye atatangulia mbele kabla ya kupewa idhini na Allaah:

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[1]

Tofauti na inavyokuwa kati ya viumbe hakuna yeyote awezaye kuomba mbele ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) isipokuwa baada ya idhini Yake.

 2 – Waombewaji wawe wapwekeshaji na waumini ambao Allaah anaridhia maneno na matendo yao:

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawamuombei yeyote yule isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.”[2]

Bi maana ambao anaridhia maneno na vitendo vyao. Sharti mbili hizo zimetajwa katika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

”Na Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao  isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa Amtakaye na kumridhia.”[3]

[1] 2:255

[2] 21:28

[3] 53:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 96-97
  • Imechapishwa: 25/01/2023