Kidini uombezi maana yake ni ukatikati katika kutatua haja kati ya yule mwenye shida na yule anayeombwa shida hiyo. Uombezi huu unakuwa mbele ya Allaah na mbele ya viumbe. Uombezi mbele ya viumbe umegawanyika sampuli mbili:

1 – Uombezi mzuri, katika mambo yenye manufaa na ambayo ni halali. Allaah (Subhaanah) amesema:

مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا

“Atakayeombea uombezi mzuri atapata fungu lake katika hayo. Na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu katika hayo… ” [1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ombeeni mlipwe thawabu. Allaah anahukumu kupitia kwa Mtume Wake kile Anachokitaka.”[2]

Huu ni uombezi mzuri ambao mtu analipwa thawabu kwayo kwa sababu unawanufaisha waislamu katika kuyatatua mambo yao na kufikia malengo yao yenye manufaa, kwa sharti kusiwe na kumshambulia au kumdhulumu yeyote.

2 – Uombezi mbaya katika kuyafikia mambo ya haramu kama vile kuondosha adhabu ya lazima. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Allaah amlaani yule mwenye kumuhifadhi mzushi. Allaah amlaani yule mwenye kubadilisha alama za ardhi.”[3]

Miongoni mwa aina za uombezi huu kunaingia vilevile uombezi kwa anayeombea zichukuliwe haki za wengine na wapewe wengine wasiostahiki. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا

“… na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu katika hayo… ”

[1] 4:85

[2] al-Bukhaariy (1432) na Muslim (2627).

[3] Muslim (1978).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 95-96
  • Imechapishwa: 25/01/2023