85. Malengo ya I´tikaaf ni kutenga muda kwa ajili ya kumwabudu Allaah

Miongoni mwa sifa za kipekee za kumi la mwisho ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf ndani yake. I´tikaaf ni kule kulazimiana na msikiti kwa ajili ya kupata muda wa kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Ni Sunnah iliyothibiti kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya I´tikaaf na Maswahabah wakafanya I´tikaaf pamoja naye na baada yake. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikaa I´tikaaf katika yale masiku kumi ya mwanzo ya Ramadhaan, kisha akakaa I´tikaaf katika masiku kumi ya katikati kisha akasema: “Nilifanya I´tikaaf katika kumi la mwanzo nikiutafuta usiku huu, kisha nikafanya katika kumi la katikati. Halafu nikajiwa na kuambiwa: “Unapatikana katika lile kumi la mwisho. Kwa hivyo yule anayependa miongoni mwenu kufanya I´tikaaf basi afanye I´tikaaf.”

Ameipokea Muslim.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf katika kumi la mwisho la Ramadhaa mpaka alipofishwa na Allaah (´Azza wa Jall) kisha wakafanya I´tikaaf wakeze baada yake.”

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwake huyohuyo tena aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf katika kila Ramadhaan siku kumi. Ulipofika ule mwaka aliyofishwa akakaa I´tikaaf siku ishirini.”

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Akaacha kukaa I´tikaaf kwa muda wa mwaka mzima. Ulipofika mwaka uliofuata akakaa I´tikaaf siku ishirini.”

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kukaa I´tikaaf anaswali Fajr kisha ndio anaingia mahali pake pa I´tikaaf. ´Aaishah akamuomba idhini na akampa idhini na kumtengenezea hema. Hafswah akamwambia ´Aaishah amuombee idhini na akafanya hivo na akamtengenezea hema. Wakati Zaynab alipoona hivo akaamrisha afanyiwe hema ambapo akatengenezewa. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoyaona mahema hayo akasema: “Nini hivi?” Wakasema: “Ni jengo la ´Aaishah, Hafswah na Zaynab.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kipi kimekupelekeeni kufanya hivo; yaondosheni nisiyaone.” Yakaondoshwa na I´tikaaf ikaachwa kufanywa ndani ya Ramadhaan mpaka akafanya I´tikaaf katika kumi la mwanzo la Shawwaal.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim katika upokezi mmoja.

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sijui kutoka kwa mwanachuoni yeyote tofauti ya kwamba I´tikaaf ni Sunnah.”

[1] 02:187

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 155-157
  • Imechapishwa: 10/03/2024