85. Haifai jilbaab kufanana na mavazi ya wanamme

Sharti ya sita ya jilbaab ni kwamba isifanane na mavazi ya wanamme. Hadiyth Swahiyh zimemlaani mwanamke anayejifananisha na wanamme, ni mamoja katika mavazi au mengine. Hapa kunafuatia baadhi ya dalili juu ya hilo:

1 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamme anayevaa mavazi ya kike na mwanamke anayevaa mavazi ya kiume.”[1]

2 – ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Si katika sisi wanawake wanaojifananisha na wanamme, wala wanamme wanaojifananisha na wanawake.”[2]

3 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanamme wenye sifa za kike na wanawake wenye sifa za kiume na akasema: ”Watoeni majumbani mwenu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtoa fulani na ´Umar pia akamtoa fulani.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanamme wenye kujifananisha na wanawake na wanawake wenye kujifananisha na wanamme.”[3]

4 – ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Watu aina tatu hawatoingia Peponi na wala Allaah hatowatazama siku ya Qiyaamah: mwenye utovu wa nidhamu kwa wazazi wake, mwanamke aliyejifanya mwanamme anayejifananisha na wanamme na duyuthi.”[4]

5 – Ibn Abiy Mulaykah (´Abdullaah bin ´Ubaydillaah) amesema:

”Kulisemwa kuambiwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa): ”Je, inafaa kwa mwanamme kuvaa ndala?” Akasema: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wanaojifananisha na wanamme.”[5]

Katika Hadiyth hizi kuna dalili ya wazi juu ya uharamu wa wanawake kujifananisha na wanamme na kinyume chake. Mbali na ile Hadiyth ya kwanza inayosema wazi vazi peke yake, nyenginezo zote ni zenye kuenea na zinahusu mavazi na mambo mengine.

[1] Abu Daawuud (2/182), Ibn Maajah (1/588), al-Haakim (4/194) na Ahmad /2/325) kupitia kwa Suhayl bin Abiy Swaalih, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Hurayrah. al-Haakim amesema:

”Swahiyh kwa sharti za Muslim.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye, mambo ni kama alivosema.

[2] Ahmad (2/199-200): ´Abdur-Razzaaq ametuhadithia: ´Umar bin Hawshab ametuhadithia: ´Amr bin Diynaar amenihadithia, kutoka kwa ´Atwaa’, kutoka kwa bwana mmoja kutokea Hudhayl ambaye amesema:

”Wakati nilipokuwa kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw, ambaye nyumba yake ilikuwa nje ya maeneo patukufu na msikiti wake ulikuwa ndani yake, alimuona Umm Sa´iyd bint Abiy Jahl ambaye alikuwa anaiga upinde na kutembea mwendo wa kiume. ´Abdullaah akasema: ”Ni nani huyu?” Bwana yule kutoka Hudhayl akasema: ”Huyu ni Umm Sa´iyd bint Abiy Jahl.” Ndipo akasema: ”Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: ”Si katika sisi wanawake wanaojifananisha na wanamme, wala wanamme wanaojifananisha na wanawake.”

[3] al-Bukhaariy (10/274), Abu Daawuud (2/305), ad-Daarimiy (2/280-281) na Ahmad (1982) kupitia kwa Hishaam ad-Dastawaa’iy, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr, kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbâs.

[4] an-Nasaa’iy (1/357), al-Haakim (1/72), al-Bayhaqiy (10/226) na Ahmad (6180) kupitia njia mbili Swahiyh kutoka kwa ´Abdullaah bin Yasaar, mtumwa wa Ibn ´Umar, kutoka kwa Saalim, kutoka kwa Ibn ´Umar. al-Haakim amesema:

”Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye, mambo ni kama alivosema.

[5] Abu Daawuud (2/184) kupitia kwa Ibn Juraydj, kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah. Wasimulizi wake ni wenye kuaminika isipokuwa Ibn Jurayj ambaye ni mudallis na haelezi amesimulia kutoka kwa nani. Licha ya hivyo ni Swahiyh kupitia Hadiyth zingine zilizokwishatangulia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 141-147
  • Imechapishwa: 17/10/2023