85. Faida ya kwanza ya kumswalia Mtume

Faida za kumswalia Mtume wa Ummah

Faida ya kwanza: Tambua ya kwamba katika aina nyingi ya du´aa za kumsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukupokelewa kutajwa Ibraahiym peke yake pasi na kuambatanishwa na jamaa zake. Bali inatajwa:

“… kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym.”

Sababu ya hilo ni kuwa katika lugha ya kiarabu ni kwamba jamaa zake mtu kunamkusanya yeye na wale wote walio chini yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ

“Allaah amemteua Aadam na Nuuh na kizazi cha Ibraahiym na kizazi cha ‘Imraan juu ya walimwengu.”[1]

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ حَاصِبًا إِلَّا آلَ لُوطٍ ۖ نَّجَّيْنَاهُم بِسَحَرٍ

“Hakika Sisi tuliwapelekea tufani ya vijiwe isipokuwa familia ya Luutw, tukawaokoa mida karibu na alfajiri.”[2]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Wasifu jamaa zake Abu Awfaa.”

Vivyo hivyo inahusiana na “watu wa nyumbani”. Allaah (Ta´ala) amesema:

رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ ۚ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ

“Rehema ya Allaah na baraka Zake ziko juu yenu enyi watu wa nyumbani. Hakika Yeye ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote, Mwenye kutukuzwa.”[3]

Kunamkusanya vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Shaykh-ul-Islaam amesema:

“Kwa ajili hiyo matamshi mengi yamekuja:

“… kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym.”

na:

“… kama Ulivyowabariki jamaa zake Ibraahiym.”

Baadhi ya matamshi yamemtaja Ibraahiym peke yake kwa sababu yeye ndiye msingi katika kusifiwa na kutakaswa na watu wengine wa nyumbani kwake ni wenye kumfuata. Baadhi ya matamshi mengine yametaja yote mawili.”

Utapoyajua haya basi utatambua kuwa wanachuoni wametilia umuhimu mkubwa kutaka kujua kushabihisha kati ya:

“… kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym.”

Kikawaida ni kwamba yule anayeshabihishwa naye huwa ni bora kuliko mshabihishwa. Lakini mambo hapa ni kinyume. Muhammad peke yake ni bora kuliko jamaa zake Ibraahiym akiwemo Ibraahiym mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam). Qadhiya ya kwamba ni bora inahusiana na kule kumsifu kulikoamrishwa ni bora kuliko sifa zote zilizokuweko na zilizoko. Kuhusu hayo wanachuoni wamejibu kwa majibu mengi, utayapata katika “Fath-ul-Baariy” (11/134-136) na “Jalaal-ul-Afhaam” (186-198). Yamefika mpaka maoni ishirini ambapo baadhi yake ni dhaifu zaidi kuliko mengine. Maoni pekee yaliyo na nguvu ni yale yaliyochaguliwa na Shaykh-ul-Islaam na Ibn-ul-Qayyim:

“Katika jamaa zake Ibraahiym kuna Mitume wasiokuweko mfano wao katika jamaa zake Muhammad. Hivyo pindipo mtu anapomuomba Allaah amsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na jamaa zake kama ambavyo anamsifu Ibraahiym na jamaa zake ambao ndani yake kuna Mitume pia, basi jamaa zake Muhammad wanapata fungu linaloendana na wao. Kwani wao hawafikii ngazi za Mitume. Ziada inayowastahiki Mitume, akiwemo Ibraahiym, sehemu inamwendea Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pia.”

Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Maelezo haya ni bora kuliko yote yaliyotangulia. Bora zaidi ni kusema kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatokana na jamaa zake Ibraahiym; bali yeye ndiye mbora wa jamaa zake Ibraahiym. ´Aliy bin Twalhah amepokea ya kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kuhusiana na maneno ya Allaah (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ

“Allaah amemteua Aadam na Nuuh na kizazi cha Ibraahiym na kizazi cha ‘Imraan juu ya walimwengu.” (03:33)

“Muhammad ni katika jamaa zake Ibraahiym.”

Hili ni andiko la wazi. Ikiwa Mitume wengine wa kizazi cha Ibraahiym wataingizwa katika jamaa zake, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana haki zaidi ya kuingia. Hivyo sentesi/jumla yetu tunaposema:

“… kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym.”

inakuwa ni kumsifu yeye na Mitume wengine kutoka katika kizazi cha Ibraahiym.

Aidha Allaah (Ta´ala) ametuamrisha kumsifu yeye na jamaa zake khususan kwa kiwango kile tunavyomsifu kwa ujumla pindi tunavyowasifu jamaa zake Ibraahiym ambao yeye ni sehemu katika wao. Kwa hivyo jamaa zake wanapata yale wanayostahiki na mengine yote yanabaki kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Amesema vilevile:

“Hapana shaka yoyote kwamba kule kuwasifu jamaa zake Ibraahiym akiwemo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja nao ni kamilifu zaidi kuliko kumsifu yeye peke yake. Kule kuombewa kusifiwa hapana shaka kwamba ni bora kuliko kule kuombewa kusifiwa kwa Ibraahiym. Hivyo inapata kufahamika faida ya ule ushabihishaji ambao unatakiwa kufahamika kimsingi wake katika hali kama hii na kwamba kumsifu kwa tamko hili ni kukubwa zaidi kuliko kumsifu kwa matamshi mengine. Kwa sababu ikiwa lengo la du´aa ni mfano wa yule anayefanana naye (ambaye naye ana fungu kubwa katika hayo), basi anapata yale yanayotakikana kwa yule aliyeshabihishwa naye zaidi kuliko aliyopata Ibraahiym na wengineo ukiongezea mafungu mengine yote ambayo hakuna mwingine yeyote amepata.

Kwa haya inapata kufahamika fadhilah zake na utukufu wake juu ya Ibraahiym na wengine wote katika jamaa zake kukiwemo ndani yake Mitume. Kwa hivyo kumsifu huku kunafahamisha na kumeandamana na ufadhilishwaji huu. Allaah amsifu na ampe amani nyingi yeye na jamaa zake. Allaah amjaze kheri kwa ajili yetu zaidi ya alivyomjaza kheri Mtume mwingine kwa ajili ya Ummah wake. Ee Allaah! Msifu Muhammad na jamaa zake Muhammad kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”[4]

[1] 03:33

[2] 54:34

[3] 11:73

[4] Jalaa’-ul-Afhaam, uk. 334-335.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 145-147
  • Imechapishwa: 03/01/2019