Miongoni mwa haki zake ambazo Allaah amewawekea katika Shari´ah waja Wake ni wao kumswalia na kumtolea salamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Mtume. Hivyo enyi walioamini mswalieni na mumsalimu kwa salamu.”[1]

Imepokelewa kwamba maana ya Allaah kumswalia ni kumsifu mbele ya Malaika Zake. Malaika kumswalia maana yake ni kumuombea du´aa. Wanadamu kumswalia ni kumuombea msamaha[2].

Katika Aayah hii ameeleza (Subhaanah) nafasi ya mja na Mtume Wake mbele Yake katika ulimwengu wa juu ya kwamba anamsifia mbele ya Malaika waliokaribu na kwamba Malaika pia wanamswalia. Kisha akaamrisha (Ta´ala) ulimwengu wa chini kumswalia na kumtolea salamu ili zikusanyike sifa juu yake kutoka kwa watu wa ulimwengu wa juu na watu wa ulimwengu wa chini. Maana ya:

وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“… mumsalimu kwa salamu.”

bi maana msalimie kwa mamkizi ya Kiislamu.

Kwa hivyo mtu anapomswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatakiwa kukusanya kati ya kumswalia na kumtolea salamu. Asifupike na kimoja wapo. Kwa msemo mwingine mtu asisemi:

‏صلى الله عليه

“Allaah mswalie.”

peke yake. Wala asisemi:

عليه السلام

“Salamu ziwe juu yake.”

peke yake. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) ameamrisha yote mawili.

Imewekwa katika Shari´ah kumswalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika zile sehemu ambazo kumesisitizwa mtu aombe ndani yake ima kwa njia ya ulazima au kwa njia ya mapendekezo yaliyosisitizwa. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ametaja katika kitabu chake “Jalaa´-ul-Afhaam” sehemu arubaini na moja. Ameanza kwa kusema:

“Sehemu ya kwanza – na ndio muhimu na iliotiliwa mkazo zaidi – katika swalah kwenye Tashahhud ya mwisho. Waislamu wameafikiana juu ya usuniwaji wake na wakatafautiana juu ya ulazima wake.”[3]

Kisha akataja sehemu nyenginezo kama mfano wa mwisho wa Qunuut, katika Khutbah kama mfano wa Khutbah ya ijumaa, ´iyd mbili, kuomba kuteremshiwa mvua, baada ya kumuitikia muadhini, wakati wa kuomba du´aa, wakati wa kuingia msikitini na wakati wa kutoka, wakati wa kumtaja (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Halafu akataja (Rahimahu Allaah) matunda yanayopatikana kwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndani yake akataja faida arubaini ambazo baadhi yake ni zifuatazo[4]:

Kutekeleza amri ya Allaah (Subhaanah) kwa jambo hilo.

Miongoni mwazo ni mswaliji kupata moja ya kumi ya swalah kutoka kwa Allaah kila anapomswalia mara moja.

Miongoni mwazo kutarajia kukubaliwa du´aa yake atapoitangulizia mbele yake.

Miongoni mwazo ni sababu ya kupata uombezi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiziambatanisha na kumuombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nafasi iliyosifiwa.

Miongoni mwazo ni kwamba ni sababu ya kusamehewa madhambi.

Miongoni mwazo ni kwamba ni sababu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuitikia yule anayemswalia na kumtolea salamu.

Ee Allaah! Msifu na msalimishe Mtume huyu mtukufu!

[1] 33:56

[2] Ameipokea al-Bukhaariy kutoka kwa Abul-´Aaliyah hali ya kuiwekea taaliki. Tazama ”Swahiyh-ul-Bukhaariy” (4797).

[3] Jalaa´-ul-Afhaam, uk. 222-223.

[4] Jalaa´-ul-Afhaam, uk. 302.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 161-162
  • Imechapishwa: 18/06/2020