Ni lazima kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kutii yale aliyoamrisha na kujiepusha na yale aliyokataza. Hayo ni katika muqtadha ya kushuhudilia ya kwamba yeye ni Mtume wa Allaah. Allaah ameamrisha kumtii katika Aayah nyingi. Mara huambatanisha na kumtii Allaah, kama pale aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.”[1]

Kuna Aayah nyenginezo mfano wake.

Mara huamrisha kumtii peke yake, kama pale aliposema:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi hakika amemtii Allaah.”[2]

وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.”[3]

Mara humtishia yule mwenye kumuasi Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama pale aliposema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[4]

Bi maana wasije kupatwa na fitina ya ukafiri, unafiki au Bid´ah kwenye mioyo yao au adhabu iumizayo duniani kwa kuuawa, kusimamishiwa adhabu ya Kishari´ah au kutiwa jela au adhabu nyenginezo za harakaharaka hapa duniani.

Allaah amefanya kumtii na kumfuata kuwa ni sababu ya mja kupendwa na Allaah na kusamehewa madhambi yake. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi; hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu.”[5]

Amefanya kumtii ndio uongofu na kumuasi ni upotevu. Amesema (Ta´ala):

وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا

”Mkimtii mtaongoka.”[6]

فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

“Wasipokuitikia basi tambua kwamba hakika wanafuata matamanio yao. Na nani mpotevu zaidi kuliko yule aliyefuata matamanio yake pasi na mwongozo kutoka kwa Allaah? Hakika Allaah hawaongoi watu madhalimu.”[7]

Amekhabarisha (Subhaanahu wa Ta´ala) kwamba yeye ndiye kiigizo chema kwa Ummah Wake. Amesema (Ta´ala):

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[8]

Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Aayah hizi tukufu ndio msingi mkubwa katika kumuiga Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maneno yake, matendo yake na hali zake. Kwa ajili hiyo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) akawaamrisha watu kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Ahzaab katika subira yake, kuvuta kwake subira, kufungamana kwake, kupambana kwake, kusubiri kwake faraja kutoka kwa Mola Wake (´Azza wa Jall) – Allaah amsifu na kumsalimisha daima mpaka siku ya malipo.”[9]

Allaah ametaja kumtii na kumfuata Mtume karibu sehemu arubaini ndani ya Qur-aan. Nafsi zinahitajia kuyajua yale aliyokuja nayo na kuyafuata zaidi kuliko wanavohitajia kula na kunywa. Kwani mtu akikosa kula na kunywa basi anafikwa na kifo hapa duniani. Lakini mtu akikosa kumtii na kumfuata Mtume anafikwa na adhabu na maangamivu ya milele.

Ameamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuiga katika kutekeleza ´ibaadah na kuzitekeleza kwa namna aliyokuwa akitekeleza. Amesema (Ta´ala):

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah.”[10]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”[11]

“Chukueni kutoka kwangu ´ibaadah zenu za hijjah.”[12]

“Mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”[13]

“Mwenye kuzipa mgongo Sunnah zangu si katika mimi.”[14]

Yako maandiko mengine mengi ambayo ndani yake kuna maamrisho ya kumuiga na vilevile kuna makatazo ya kwenda kinyume naye.

[1] 04:59

[2] 04:80

[3] 24:56

[4] 24:63

[5] 03:31

[6] 24:54

[7] 28:50

[8] 33:21

[9] Tafsiyr ya Ibn Kathiyr (03/475).

[10] 33:21

[11] al-Bukhaariy (631).

[12] Abu Daawuud (1970) na an-Nasaa´iy (3063).

[13] Muslim (4468).

[14] al-Bukhaariy (4776) na Muslim (1401).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 158-160
  • Imechapishwa: 18/06/2020