84. Sura ya nne: Fadhilah za watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yaliyo ya wajibu kwao pasi na kuzembea wala kuchupa mipaka

Watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jamaa zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao swadaqah imeharamika juu yao. Nao ni kizazi cha ´Aliy, kizazi cha Ja´far, kizazi cha ´Aqiyl, kizazi cha al-´Abbaas, Banuu al-Haarith bin ´Abdil-Muttwalib na wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watoto wake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

“Hakika si vyenginevyo Allaah anachotaka ni kukuondosheeni maovu, watu wa nyumba, na akutakaseni mtakaso ukweli wa kuwatakasa.”[1]

Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Jengine ambalo halina mashaka yoyote kwa yule mwenye kuizingatia Qur-aan ni kwamba wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaingia ndani ya maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

“Hakika si vyenginevyo Allaah anachotaka ni kukuondosheeni maovu, watu wa nyumba, na akutakaseni mtakaso ukweli wa kuwatakasa.”

Mtiririko wa maneno unawazungumzia wao. Ndio maana baada ya haya yote akasema:

وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ

“Kumbukeni yale yanayosomwa kweniye majumbani yenu katika Aayah za Allaah na hekima.”[2]

Yafanyieni kazi yale ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anamteremshia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika nyumba zenu katika Qur-aan na Sunnah. Haya yamesemwa na Qataadah na wengineo.

Kumbukeni neema hii ambayo nyinyi mmefanywa ni maalum kwayo kati ya watu wote ambapo Wahy unateremka katika majumba yenu mbali na watu wengine wote. ´Aaishah as-Swiddiyqah bint wa as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ndiye wa kwanza kwa neema hii na ndiye kafanywa maalum zaidi kwa neema hii kubwa. Kwani hakuna yeyote Wahy ulimteremkia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenye kitanda cha mwanamke isipokuwa yeye tu, kama alivoelezea hilo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadhi ya wanachuoni wamesema: “Kwa sababu hakuoa mwanamke bikira mwengine zaidi yake na hakuna mwanamume yeyote aliyelala pamoja naye isipokuwa tu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo anastahiki kufanywa maalum kwa sifa hii na kupwekeshwa kwa nafasi hii ya juu. Lakini ikiwa wakeze wanaingia katika watu wa familia yake basi nduguze wana haki zaidi ya jina hilo.”[3]

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanawapenda watu wa nyumbani kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanajenga urafiki nao na wanachunga wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu yao pale aliposema siku ya Ghadiyr Khumm[4]:

“Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumbani kwangu.”[5]

Ahl-us-Sunnah wanawapenda na wanawakirimu. Kwa sababu kufanya hivo ni katika kumpenda na kumkirimu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hilo ni kwa sharti wawe ni wenye kufuata Sunnah na wenye msimamo juu ya dini, kama walivokuwa watangu wao kama mfano wa al-´Abbaas na watoto wake. Kuhusu wale wenye kwenda kinyume na Sunnah na wasinyooke juu ya dini haijuzu kuwapenda ijapokuwa ni katika watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hiyo msimamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah inapokuja kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni msimamo wa kati na kati na uadilifu. Wanawapenda wale walioshikamana na wenye msimamo na dini katika wao. Sambamba na hilo wanajiweka mbali na wale waliokwenda kinyume na kupinda mbali na dini hata kama ni katika watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuwa kwake ni katika watu wa familia na nduguze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumfai chochote mpaka awe na msimamo katika dini. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia akisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoteremshiwa:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ

“Waonye jamaa zako wa karibu.”[6]

alisimama na kusema:

“Enyi Quraysh! – au maneno mfano wa hayo – Ziuzeni nafsi zenu! Hakika mimi sintokunufaisheni mbele ya Allaah na chochote. Ee ´Abbaas, ami ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Sintokunufaisha mbele ya Allaah na chochote. Ee Swafiyyah, shangazi yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Sintokunufaisha mbele ya Allaah na chochote. Ee Faatwimah, binti ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Niombe katika mali utakacho! Hakika mimi sintokunufaisheni mbele ya Allaah na chochote.”[7]

Vilevile imepokelewa katika Hadiyth:

“Yule aliyecheleweshwa na matendo yake hatoharakishwa na ukoo wake.”[8]

Vilevile Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye kujiweka mbali na mfumo wa Raafidhwah ambao wamechupa mipaka kwa baadhi ya watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakadai kuwa wamekingwa na kukosea kama ambavo wanajiweka mbali pia na mfumo wa Nawaaswib ambao wananasibisha uadui na kuwatukana watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao wana msimamo mzuri wa dini. Vilevile ni wenye kujiweka mbali na mfumo wa watu wa Bid´ah na makhurafi ambao wanafanya Tawassul kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanafanya waungu badala ya Allaah.

Katika maudhui haya na mengineyo Ahl-us-Sunnah wanafuata mwenendo wa kati na kati na njia ilionyooka isiyokuwa ndani yake na kuzembea wala kuchupa mpaka kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo. Watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wenye msimamo mzuri wa dini wanakaripia kuchupa mpaka juu yao na ni wenye kujitenga mbali na wachupaji mpaka. Kiongozi wa waumini, ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) aliwachoma moto wachupaji mpaka waliovuka mpaka juu yake na akawachoma kwa moto. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) akakubaliana naye juu ya kuwaua. Lakini hata hivyo yeye alionelea vyema kuwaua kwa upanga badala ya kuwatia moto. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimtafuta ´Abdullaah bin Sabaa´ – ambaye ndiye kiongozi wa wachupa mpaka – ili amuue, lakini hata hivyo akakimbia na kujificha.

[1] 33:33

[2] 33:34

[3] Tafsiyr ya Ibn Kathiyr (03/487).

[4] Ghadiyr Khumm ni jina la maeneo.

[5] Muslim (6175).

[6] 26:214

[7] al-Bukhaariy (2753) na Muslim (503).

[8] Muslim (6793).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 163-165
  • Imechapishwa: 18/06/2020