Hakuna ubaya kubainisha nafasi yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa yale aliyomsifu kwayo Allaah na kutaja nafasi yake ambayo Allaah amemfadhilisha kwayo na mtu akaamini jambo hilo. Hakika yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana nafasi ya juu ambayo Allaah amempa. Yeye ni mja na Mtume wa Allaah. Yeye ndiye kiumbe mwenye kheri zaidi katika viumbe Wake. Yeye ndiye kiumbe mbora kabisa katika viumbe Wake. Yeye ni Mtume wa Allaah kwenda kwa watu wote na kwenda kwa majini na watu. Yeye ndiye Mtume mbora. Yeye ndiye Nabii wa mwisho na hakuna Nabii mwingine baada yake. Allaah amekifungua kifua chake, akalinyanyua jina lake na akajaalia udhalili na unyonge kwa yule mwenye kwenda kinyume na amri yake. Yeye ndiye mwenye nafasi yenye kusifiwa ambayo Allaah (Ta´ala) amesema juu yake:

عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا

“Hapana shaka Mola wako atakuinua cheo chenye kufisika.”[1]

Nafasi ambayo Allaah atamtunuku kwa ajili ya kuwaombea watu siku ya Qiyaamah ili Mola wao kuwapumzisha kutoka kwenye kisimamo kizito. Hicho ni cheo maalum kwake yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na Mitume wengine.

Yeye ndiye kiumbe anayemcha na kumuogopa Allaah zaidi. Allaah amekataza kunyanyua sauti mbele yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawasifu wale wenye kuziteremsha sauti zao mbele yake. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ إِنَّ الَّذِينَ يَغُضُّونَ أَصْوَاتَهُمْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ امْتَحَنَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ لِلتَّقْوَىٰ ۚ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ إِنَّ الَّذِينَ يُنَادُونَكَ مِن وَرَاءِ الْحُجُرَاتِ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ وَلَوْ أَنَّهُمْ صَبَرُوا حَتَّىٰ تَخْرُجَ إِلَيْهِمْ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Enyi walioamini! Msinyanyue sauti zenu juu ya sauti ya Nabii na wala msiseme naye kwa sauti ya juu, kama mnavyosemezana wenyewe kwa wenyewe kwa sauti za juu; yasije kuporomoka matendo yenu ilihali hamhisi. Hakika wale wanaoteremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Allaah, hao ndio ambao Allaah amezitahini nyoyo zao kwa ajili ya uchaji; watapata msamaha na ujira mkuu. Hakika wale wanaokuita nyuma ya vyumba, wengi wao hawatii akilini. Endapo kwamba wao wangesubiri mpaka ukawatokea, bila shaka ingelikuwa ni kheri kwao. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Allaah amewaadabisha waja Wake waumini kupitia Aayah hizi  kuhusu namna wanavyotakiwa kutangamana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kumuheshimu, kumtukuza na kumuadhimisha… Hawatakiwi kuzinyanyua sauti zao mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya sauti yake.”[3]

Vilevile Yeye (Subhaanah) amekataza kumwita Mtume kwa jina lake kama wanavoitwa watu wengine. Kama vile kusema “Ee Muhammad!” Anatakiwa kuitwa kwa njia ya utume na unabii kama kusema “Ee Mtume wa Allaah! Ee Nabii wa Allaah!” Amesema (Ta´ala):

لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا

“Msifanye wito wa Mtume kati yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi.”[4]

Ni kama ambavo Allaah Mwenyewe anamwita kwa njia ya “Ee Nabii! Ee Mtume!” Allaah na Malaika Wake wamemswalia na akawaamrisha wamswalie na kumtolea salamu. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Mtume. Hivyo enyi walioamini mswalieni na mumtakie amani.”[5]

Lakini hakutengwi wakati wala namna maalum ya kumsifu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa kwa dalili sahihi kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Yale yanayofanywa na watu wa maulidi kutenga siku maalum ambayo wanadai kuwa ndio siku aliyozaliwa ni Bid´ah yenye kukemewa.

Miongoni mwa kumuadhimisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuziadhimisha Sunnah zake, kuamini kuwa ni lazima kuzitendea kazi na kwamba zinachukua nafasi ya pili baada ya Qur-aan inapokuja katika ulazima wa kuziadhimisha na kuzitendea kazi. Kwa sababu ni Wahy kutoka kwa Allaah (Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.”[6]

Kwa hivyo haijuzu kuzitilia mashaka, kulidogesha jambo lake, kuzizungumzia kwa njia ya kusahihisha au kudhoofisha njia zake au cheni za wapokezi wake au kufafanua maana zake isipokuwa kwa elimu na uhifadhi. Ni jambo limekithiri hii leo wajinga kuwa na ulimi mrefu juu ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) khaswakhaswa baadhi ya vijana ambao bado wanakua ambao bado ndio wako katika hatua ya kwanza ya masomo. Matokeo yake wakawa wanazisahihisha na kuzidhoofisha Hadiyth na wanawajeruhi wapokezi bila ya elimu mbali na kusoma vitabu. Jambo hili ni khatari kubwa juu yao na juu ya Ummah. Ni lazima kwao kumcha Allaah na kusimama katika mpaka wao.

[1] 17:79

[2] 49:02-05

[3] Tafsiyr ya Ibn Kathiyr (04/206).

[4] 24:63

[5] 33:56

[6] 53:03-04

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 155-157
  • Imechapishwa: 16/06/2020