Kupindukia ni kuchupa mipaka. Amesema (Ta´ala):

لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ

”Msipindukie mipaka katika dini yenu.”[1]

Bi maana msivuke kiwango.

al-Itwraa´ ni kupindukia katika kusifu na kuchanganya na uongo. Makusudio ya kuchupa mipaka juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuvuka mpaka katika nafasi yake kwa kumnyanyua juu zaidi ya kiwango cha uja na utume na kumfanyia kitu katika aina za ´ibaadah kwa njia ya kumuomba, kumtaka msaada badala ya Allaah na kuapa kwa jina lake. Makusudio ya kumsifu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kupindukia ni kuzidisha katika kumsifu. Alikataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokamana na jambo hilo pindi aliposema:

“Msinifu kwa kupitiliza kama walivyopindukia wakristo kwa ´Iysaa bin Maryam. Hakika mimi ni mja. Hivyo semeni “Mja wa Allaah na Mtume Wake.”[2]

Bi maana msinifu kwa batili na wala msivuki mipaka katika kunisifu kama wakristo walivyochupa mipaka kwa ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na matokeo yake wakadai kuwa ni mungu. Nisifuni kama alivyonisifu Mola wangu na semeni: “Mja na Mtume wa Allaah”.

Wakati baadhi ya Maswahabah zake walipomwambia: “Wewe ni bwana wetu.” Akasema: “Bwana ni Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).” Pindi waliposema: “Wewe ni mbora wetu kwa ubora na ni mkubwa wetu kwa ukarimu.” Akasema: “Semeni msemayo, au baadhi yake tu, na wala asikupotezeni shaytwaan.”[3]

Kuna watu walimwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Ee mbora wetu, mtoto wa mbora wetu na bwana wetu na mtoto wa mbora wetu.” Akasema: “Enyi watu! “Semeni msemayo na wala asikupotezeni shaytwaan. Mimi ni Muhammad, mja na Mtume wa Allaah. Sipendi mnipandishe juu zaidi ya nafasi aliyonipandisha Allaah (´Azza wa Jall).”

Alichukia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumsifu kwa matamshi kama haya “Wewe ndiye bwana wetu. Wewe ndiye mbora wetu. Wewe ndiye mtukufu wetu” pamoja na kwamba yeye ndiye mbora na mtukufu zaidi wa viumbe pasi na shaka yoyote. Lakini aliwakataza kufanya hivo kwa ajili ya kuwaepusha na uchupaji mipaka na kupitiliza katika kumsifu. Sababu nyingine ni kwa sababu ya kuilinda Tawhiyd. Badala yake akawaelekeza wamsifu kwa sifa mbili ambazo ndio tukufu zaidi kwa mja na ndani yake hazina uchupaji mipaka wala khatari juu ya ´Aqiydah. Sifa zenyewe ni “Mja na Mtume wa Allaah”. Hakupenda wampandishe zaidi ya cheo chake alichopandishwa na Allaah (´Azza wa Jall) katika cheo alichomridhia.

Watu wengi wamekwenda kinyume na makatazo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matokeo yake wakawa wanamuomba yeye, wanamtaka msaada, wanaapa kwa jina lake na wanamuomba mambo ambayo hayaombwi kutoka kwa yeyote isipokuwa Allaah pekee, kama inavofanywa katika maulidi, mashairi na Anaashiyd. Hawapambanui kati ya haki ya Allaah na haki ya Mtume. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema katika an-Nuuniyyah:

Allaah ana haki isiyomwendea mwengine

mja pia ana haki – zinakuwa haki mbili

Hivyo usizifanye haki mbili hizo kuwa haki moja

pasi na kupambanua wala kutofautisha.

[1] 04:171

[2] Ahmad (1635), Abu Daawuud (4807) na tamko ni lake.

[3] Ahmad (13553).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 153-155
  • Imechapishwa: 16/06/2020