Ni lazima kwa mja kwanza kumpenda Allaah (´Azza wa Jall). Ni miongoni mwa aina kubwa kabisa za ´ibaadah. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ

“Wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah.”[1]

Kwa sababu Yeye ndiye Mola ambaye amewatunuku waja Wake wote kwa aina mbalimbali za neema zenye kuonekana na zilizojificha.

Kisha baada ya kumpenda Allaah (Ta´ala) ni lazima kumpenda Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye alilingania kwa Allaah, akamtambulisha, akaifikisha Shari´ah Yake na akabainisha hukumu Zake. Hakuna kheri yoyote ya duniani na Aakhirah iliyowafikia waumini isipokuwa ilikuwa kupitia mikononi mwa Mtume huyu. Hakuna yeyote atakayeingia Peponi isipokuwa kwa kumtii na kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imekuja katika Hadiyth:

“Mambo matatu yakipatikana kwa mtu hupata utamu wa imani; Allaah na Mtume Wake wawe ni wenye kupendwa zaidi kwake kuliko yeyote yule, ampende mtu na asimpendei jengine isipokuwa iwe ni kwa ajili ya Allaah na achukie kurudi katika ukafiri baada ya Allaah kumwokoa nao kama anavyochukia kutupwa ndani ya Moto.”[2]

Mapenzi ya kumpenda Mtume yanafuatia mapenzi ya kumpenda Allaah (Ta´ala), ni yenye kulazimiana na ndio yanashika nafasi ya pili. Mapenzi ya kumpenda (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yamekuja kwa njia maalum na ulazima wa kuyatanguliza mbele ya mapenzi ya wapendwa wote isipokuwa Allaah (Ta´ala). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatoamini mmoja wenu mpaka niwe ni mwenye kupendwa zaidi kwake kuliko mtoto wake, baba yake na watu wote.”[3]

Bali imepokelewa kwamba ni lazima kwa muumini ampende Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zaidi kuliko anavyoipenda nafsi yake mwenyewe. Imekuja katika Hadiyth kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika wewe unapendwa zaidi kwangu kuliko kila kitu isipokuwa tu nafsi yangu.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ninaapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake mpaka niwe ni mwenye kupendwa zaidi kwako kuliko hata nafsi yako.” Ndipo ´Umar akasema: “Hivi sasa wewe unapendwa zaidi kwangu kuliko nafsi yangu.” Akasema: “Hivi sasa ´Umar.”[4]

Hapa tunajifunza kuwa mapenzi ya kumpenda Mtume yanakuwa ya lazima na ni yenye kutangulizwa mbele mbele ya kila kitu isipokuwa tu mapenzi ya kumpenda Allaah. Kwani yenyewe ni yenye kufuatia na ni yenye kwenda sambamba nayo. Kwa sababu inahusiana na kupenda kwa ajili ya Allaah. Yanazidi kwa kuzidi kumpenda Allaah ndani ya moyo wa muumini na yanapungua kwa kupungua kwake. Kila anayempenda mtu kwa ajili ya Allaah basi anampenda kwa ajili Yake.

Kumpenda (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunapelekea kumuadhimisha, kumtukuza, kumfuata kuyatanguliza maneno yake mbele ya maneno ya kiumbe yeyote na kuziadhimisha Sunnah zake. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mapenzi yote ya kumpenda na kumtukuza mtu yanajuzu kwa kufuatia kumpenda na kumtukuza Allaah. Kama kumpenda na kumtukuza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni katika ukamilifu wa mapenzi ya kumpenda na kumtukuza Aliyemtuma. Ummah wake wanampenda kwa sababu ya Allaah kumpenda na wanamuadhimisha na kumtukuza kwa sababu ya Allaah kumtukuza. Kwa hiyo ni mapenzi kwa ajili ya Allaah na ni katika mambo yanayowajibisha mapenzi ya Allaah.

Kinachokusudiwa ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Allaah ameweka juu yake haiba na watu kumpenda… Kwa ajili hiyo hakukuwepo kiumbe anayependwa zaidi kwa viumbe, mwenye haiba zaidi na mwenye kutukuzwa zaidi vifuani kuliko Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenye vifua vya Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). ´Amr bin al-Aasw amesema baada ya kusilimu kwake:

“Hakukuweko mtu anayechukizwa zaidi kuliko yeye. Wakati niliposilimu hakukuweko mtu ninayempenda zaidi na kutukuzwa zaidi machoni mwangu kuliko yeye. Lau mtu aniulize kumsifia basi nilikuwa siwezi kwa sababu nilikuwa siwezi kujaza macho yangu kumtazama kutokana na nilivyokuwa namtukuza.”

´Urwah bin Mas´uud amesema kuwaambia Quraysh:

“Enyi watu wangu! Nimeshawazungukia Kisraa, Qaysar na wafalme mbalimbali na sijaona mfalme yeyote ambaye anatukuzwa zaidi na watu wake kama Maswahabah wa Muhammad wanavyomtukuza Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ninaapa kwa Allaah wanashindwa kumtazama usoni mwake kwa sababu ya kumtukuza. Hatemi mate isipokuwa yataanguka mikononi mwa mmoja wao na wanajifuta kwayo nyusoni na vifuani mwao. Anapotawadha basi wanakaribia kuuana kutokana na wudhuu´ wake.”[5]

[1] 02:165

[2] al-Bukhaariy (21) na Muslim (163).

[3] al-Bukhaariy (21) na Muslim (163).

[4] al-Bukhaariy (6632).

[5] Jalaa´-ul-Afhaam, uk. 120-121.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 151-153
  • Imechapishwa: 16/06/2020