Sijui mwanachuoni yeyote anayesema matendo kama du´aa, kumuombea msamaha, swadaqah, kulipa madeni na kutekeleza mambo ya wajibu hayamfikii yule maiti. Wanachuoni wengi wamesimulia maafikiano juu ya hilo. Kuna wanachuoni wengi wameshurutisha hicho kitendo cha wajibu kiweze kufanywa na mtu mwingine pindi yuko hai ili kiweze kumfikia kama maiti. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.” (59:10)”

Baada ya Maswahabah mpaka siku ya Qiyaamah:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi tambua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na [omba msamaha] kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike!” (47:19)

Pindi Abu Salamah alipofariki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuombea. Kadhalika alimuombea yule maiti aliyemswalia swalah ya jeneza. Allaah alimuwekea katika Shari´ah yeye na kila anayemswalia maiti aseme “Ee Allaah! Mghufurie. Mrehemu. Muafu. Msamehe.” Du´aa hii inajulikana.

Kuhusu kufikiwa na ´ibaadah za kimali kama kuachia mtumwa huru na swadaqahh wanachuoni wengi katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa thawabu zake zinamfikia yule maiti kama jinsi anavyofikiwa na du´aa na kuombewa msamaha.

Ama kufikiwa na ´ibaadah za kimwili kama vile swawm, swalah na kisomo cha Qur-aan maoni sahihi ni kwamba zinamfikia pia. Haya ndio maoni yaliyo na madhehebu ya Imaam Ahmad, Abu Haniyfah na kundi katika Shaafi´iyyah na Maalikiyyah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 177-178
  • Imechapishwa: 20/11/2016