Twaaghuut ni kila ambacho mja anakivukia mipaka katika vinavyoabudiwa, kufuatwa au kutiiwa[1]. Kila chenye kwenda kinyume na Shari´ah ni Twaaghuut. Kimeitwa kuwa ni “Twaaghuut” kutokamana na neno Twughyaan, nayo maana yake ni kuvuka mpaka.

Maana ya kukufuru Twaaghuut ni wewe kujitenga mbali na ´ibaadah anayofanyiwa asiyekuwa Allaah, ukaikanusha, kuichukia, kujenga uadui na kuwajengea uadui wenye nayo. Kukufuru Twaaghuut ni kujitenga na kila chenye kuabudiwa badala ya Allaah, kukanusha kila ´ibaadah anayofanyiwa asiyekuwa Allaah, kuikanusha, kuichukia, kuwachukia wenye nayo na kuwajengea uadui. Hii ndio maana ya kukufuru Twaaghuut. Ni wewe kujiweka mbali na shirki aina zote na kila dini isiyokuwa ya Kiislamu, uikemee, uikanushe, uichukie, uinjengee uadui na uwanjee uadui wenye nayo. Hili ni mosi.

Pili ni kumuamini Allaah. Utapofanya mambo mawili haya basi wewe ni mpwekeshaji. Bi maana ukakufuru Twaaghuut na kumuamini Allaah. Hii ndio maana ya “hakuna mungu isipokuwa Allaah”. Maana yake ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Hii ndio kalima ya Tawhiyd. Hili ndio neno la Tawhiyd linalomkinga mwenye nalo na shirki. Ndio neno ambalo kwa ajili yake Allaah amewatuma Mitume, akawagawanya watu kati ya waangamivu na wenye furaha, kukasimama Jihaad, kukasimama Qiyaamah na kwa ajili yake kukaumbwa Pepo na Moto[2].

“Hakuna mungu isipokuwa Allaah” maana yake ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah[3]. Neno “hakuna mungu isipokuwa Allaah” ndani yake mna mambo mawili:

1 – Kufuru.

2 – Imani.

“Hakuna mungu… “

Huku ni kuikufuru Twaaghuut.

“… isipokuwa Allaah.”

Huku ni kumuamini Allaah.

“Hakuna mungu… ” huku ni kukanusha aina zote za ´ibaadah anazofanyiwa asiyekuwa Allaah na ndio maana ya kukufuru Twaaghuut.

“…. isipokuwa Allaah” unamthibitishia Allaah (´Azza wa Jall) aina zote za ´ibaadah. Huku ndio kumwamini Allaah.

[1] I´laam-ul-Muwaqqi´iyn (01/35)

[2] Zaad-ul-Ma´aad (01/05) na “Fath-ul-Majiyd” (01/75)

[3] Fath-ul-Majiyd (01/121)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 09/04/2023