Mfungaji hafungui kwa kupaka wanja au dawa za machoni hata kama atahisi ladha yake kooni mwake. Kwa sababu mambo hayo sio kula, kunywa wala hayana maana ya viwili hivyo.

Vilevile hafungui kwa kuweka ndani ya sikio lake, wala hafungui kwa kuweka dawa kwenye kidonda hata kama atahisi ladha ya dawa hiyo kooni mwake. Kwa sababu kufanya hivo sio kula, kunywa wala hakuleti maana ya kula na kunywa. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika kitabu chake “Haqiyqat-us-Swiyaam”:

“Tunajua kuwa hakuna ndani ya Qur-aan na Sunnah yanayofahamisha juu ya kufungua kwa mambo haya. Hivyo basi, tukajua kuwa havifunguzi. Hakika swawm ni katika dini ya waislamu ambayo msomi na mtu wa kawaida wote wawili wanahitaji kuijua.”

Yangelikuwa mambo haya ni miongoni mwa mambo aliyoharamisha Allaah na Mtume Wake juu ya swawm na pia funga inaharibika kwayo, basi ingelikuwa ni lazima kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuyabainisha mambo hayo. Mambo hayo yangelitajwa basi wangeliyajua Maswahabah na wakawafikishia nayo ummah kama walivyowafikishia mambo mengine ya Shari´ah. Pindi hakuna mwanachuoni yeyote aliyeyanakili kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – si Hadiyth Swahiyh, dhaifu, Hadiyth ilioungana cheni ya wapokezi au Hadiyth ambayo kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi – basi ndipo ikatambulika kuwa hakuna chochote kilichotajwa katika mambo hayo. Hadiyth zilizosimuliwa kuhusu wanja, kwa maana nyingine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kutia wanja wa dawa wakati wa kulala na akasema:

“Lengo ni ili ajilinde nayo mfungaji.”

ni dhaifu. Ameipokea Abu Daawuud katika “as-Sunan” yake na hakuna mwingine aliyeipokea. Abu Daawuud amesema:

“Yahyaa bin Ma´iyn amenambia kuwa Hadiyth hii ni munkari.”

Shaykh-ul-Islaam pia amesema:

“Ni lazima kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwabainishia ummah hukumu ambazo wanahitaji kuzitambua ubainifu wenye kuenea na ingelilazimika ummah kulinakili. Ikiwa hilo halikupatikana basi itatambulika kuwa sio katika dini.”

Ni maneno imara yaliyojengeka juu ya hoja za wazi na misingi iliyothibiti.

Mfungaji hafungui kwa kuonja chakula asipokimeza wala hafungui kwa kunusa manukato na uvumba. Lakini asivute kwa ndani ya pua moshi wa uvumba kwa sababu ina rutuba zinazopanda. Pengine kitu katika chakula kikafika tumboni. Mfungaji hafungui vilevile kwa kusukutua mdomo na kupandisha maji puani. Lakini asipalizie kwa kishindo kwa sababu huenda maji kidogo yakapenyeza na kuingia tumboni mwake. Laqiytw bin Swabirah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanya kishindo katika kuyapindisha maji puani isipokuwa ukiwa umefunga.”

Ameipokea Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na ameisahihisha Ibn Khuzaymah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 108-110
  • Imechapishwa: 04/03/2024