Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

69 – Safari ya kupandishwa mbinguni ni haki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisafirishwa kwa kupandishwa mbinguni sehemu ya usiku. Safari hiyo ilikuwa katika hali ya kuwa macho na si ndotoni. Kisha akampandisha kule anakotaka Allaah. Allaah akamkirimu kwa yale anayotaka na akamfunulia yale anayoyataka kumfunulia:

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ

“Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.”[1]

Allaah amsifu na amsalimishe duniani na Aakhirah.

MAELEZO

Jibriyl alimsafirisha sehemu ya usiku Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa amri ya Allaah kutoka msikiti Mtakatifu kwenda msikiti wa al-Aqswaa:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake [amechukuliwa] ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote daima, Mwenye kuona yote daima.”[2]

Safari hii ni miongoni mwa miujiza yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kikawaida safari kama hii ilikuwa inachukua muda usiopungua mwezi mmoja (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alienda ndani ya usiku mmoja.

Kuhusu safari ya kupandishwa mbinguni, kunamaanishwa kupandishwa juu, ni kama:

تَعْرُجُ الْمَلائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ

“Malaika na Roho [Jibrily] wanapanda Kwake katika siku kiasi chake ni miaka elfu khamsini.”[3]

Yote mawili yamethibiti kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kusafirishwa sehemu ya usiku ilikuwa kutoka msikiti Mtakatifu kwenda msikiti wa al-Aqswaa, kuhusu safari ya kupandishwa mbinguni ilikuwa kutoka ardhini kwenda mbinguni. Yote haya yametokea ndani ya usiku mmoja. Alipofika Yerusalemu aliwaswalisha Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) kisha akapandishwa mbinguni. Alivuka mbingu ya saba na Allaah akamuonesha alama kubwa. Kisha Jibriyl akamteremsha ardhini mahali palepale walipoanza safari yao ya kupanda mbinguni katika usiku huohuo mmoja. Kusafirishwa usiku kumetajwa katika Suurah “al-Israa” na kupandishwa mbinguni kumetajwa katika Suurah “an-Najm”:

وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ

“Naapa kwa nyota zinapotua. Hakupotoka swahibu wenu na wala hakukosea. Wala hatamki kwa matamanio yake. Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa. Amemfunza mwenye nguvu madhubuti.”[4]

Bi maana Jibriyl (´alayhis-Salaam).

ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ وَهُوَ بِالْأُفُقِ الْأَعْلَىٰ ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ أَوْ أَدْنَىٰ

”Mwenye muonekano mzuri na akalingamana sawasawa. Naye yuko juu kabisa katika upeo wa macho, kisha akakurubia na akashuka, kisha akawa kiasi cha umbali wa mipinde miwili au karibu zaidi.”[5]

Ima yeye alisogea karibu na Mola wake (Subhanaahu wa Ta´ala) au Jibriyl alisogea karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hivyo safari ya usiku na kupandishwa mbinguni ni haki. Yule mwenye kuyapinga au akaona kuwa ni mambo yako mbali amemkufuru Allaah (´Azza wa Jall), na ambaye atayapindisha maana ni mpotofu. Hakuna walioyapinga isipokuwa tu washirikina. Ambaye atasema kuwa alisafirishwa kwa roho, pasi na kiwiliwili chake, au kwamba ilikuwa ni usingizini ni mpotofu. Kwa sababu Allaah amesema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku… “

Mja ni yule mwenye roho na kiwiliwili. Haisemwi kuwa roho peke yake ni mja.  Safari hiyo ilikuwa katika hali ya kuwa macho na haikuwa usingizini. Hakuna mazingatio yanayopatikana usingizini. Kila mtu anakuwa na ndoto za ajabu na sio Mtume peke yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtunzi wa kitabu amesema:

“Safari hiyo ilikuwa katika hali ya kuwa macho na si ndotoni.”

Hapa wanaraddiwa wale wanaosema kwamba alisafiri kwa roho yake. Bali alisafiri yeye kama yeye, kwa msemo mwingine ilikuwa kwa kiwiliwili na kiroho. Kwani Allaah amesema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku… “

[1] 53:11

[2] 17:1

[3] 70:4

[4] 53:1-5

[5] 53:6-9

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 88-90
  • Imechapishwa: 23/01/2023