Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msirudi baada yangu kuwa makafiri wapotevu baadhi wakizikata shingo za wengine.”[1]

“Pindi waislamu wawili watapokutana na silaha zao yule muuaji na yule muuliwaji Motoni.”[2]

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumuua ni ukafiri.”[3]

“Yule mwenye kumwambia nduguye “ee kafiri”, basi imemgusa mmoja wao.”[4]

“Ni kumkufuru Allaah mtu kuikana nasabu yake hata kama imefichikana.”[5]

Hizi na Hadiyth mfano wake ambazo ni Swahiyh na zimehifadhiwa tunajisalimisha nazo ijapokuwa hatuzielewi. Hatuzizungumzii, hatujadiliani nazo na wala hatuzifasiri kwa njia inayopingana na uinje wake. Hatuzirudishi isipokuwa kwa kitu kilicho na haki zaidi ya kukipokea.”

MAELEZO

Maana yake ni kwamba ukafiri umegawanyika sampuli mbili:

1 – Ukafiri unaomtoa mtu katika dini.

2 – Ukafiri wa kimatedo usiomtoa mwenye nao katika dini. Ukafiri katika maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msirudi baada yangu kuwa makafiri wapotevu baadhi wakizikata shingo za wengine.”

ni wa kimatendo. Kwa sababu waumini kupigana vita vya wao kwa wao, kutokana na tafsiri, hakuwatoi katika dini. Allaah (´Azza wa Jall) amesema kuhusu waasi:

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao, lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni vita na lile ambalo linakandamiza mpaka lielemee katika amri ya Allaah; likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu na fanyeni haki. Hakika Allaah anapenda wafanyao haki. Hakika waumini ni ndugu. Suluhisheni baina ya ndugu zenu [waliotofautiana] na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”?[6]

Vivyo hivyo kuhusu Hadiyth:

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumuua ni ukafiri.”

Ukafiri kama huu ni wa kimatendo usiomtoa mwenye nao katika Uislamu muda wa kuwa hajalalisha dhambi yake; katika hali hiyo itakuwa ni ukafiri mkubwa.

Ukafiri mkubwa ambao unamtoa mwenye nao katika Uislamu ni ule unaohusiana na kumwabudu mwengine asiyekuwa Allaah, kuonelea kuwa sheria zilizotungwa na watu ni bora kuliko hukumu ya Allaah na aina nyenginezo za ukafiri mkubwa kama vile ukafiri wa kukadhibisha, ukafiri wa kufanya ukaidi, ukafiri wa kufanya kiburi, ukafiri wa kukanusha, ukafiri wa unafiki, ukafiri wa kutia shaka, ukafiri wa kupuuza na ukafiri wa kuritadi. Ukafiri uliyotajwa katika Hadiyth zilizopo hapo juu ni ukafiri wa kimatendo usiomtoa mwenye nao katika Uislamu. Hazitakiwi kufasiriwa kwa tafsiri za batili wala kuzipindisha maana; bali zinatakiwa kufasiri kwa maana sahihi zinazoenda sambamba na Qur-aan na Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kumwambia nduguye “ee kafiri”, basi imemgusa mmoja wao.”

Ikiwa anakusudia ukafiri mkubwa na yule mwambiwaji kweli ni kafiri mwenye ukafiri mkubwa, basi mambo ni kama alivosema mzungumzaji. Na ikiwa mambo si kama alivosema mzungumzaji, basi ukafiri mkubwa huo unamrejelea yeye mwenyewe – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] al-Bukhaariy (121) na Muslim (65).

[2] al-Bukhaariy (31) och Muslim (2888).

[3] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

[4] al-Bukhaariy (6104) na Muslim (60).

[5] Ahmad (2/215). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (4485).

[6] 49:09

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 170-172
  • Imechapishwa: 28/06/2026