79. Jilbaab ni lazima iwe yenye kupwaya na pana

Sharti ya nne ya jilbaab ni kwamba inapaswa iwe pana na isiwe yenye kubana ambapo ikaonyesha kitu katika maumbo yake ya mwili. Kwa sababu lengo la nguo ni kuondosha fitina, jambo ambalo halifikiwi isipokuwa kwa nguo iliyopwaya na pana. Kuhusu nguo yenye kubana, hata kama itafunika rangi ya ngozi, inaonyesha maumbo ya mwili wake au baadhi ya maumbo yake, jambo ambalo linapelekea katika maharibifu. Kwa hivyo ni lazima iwe yenye kupwaya. Usaamah bin Zayd amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinipa nguo ya kikoptiki nene, nguo nene aliyopewa zawadi na Dihyah al-Kalbiy. Nikampa nayo mwanamke wangu ambapo akasema: ”Ni kwa nini hukuvaa ile nguo ya kikoptiki?” Nikasema: ”Nimempa nayo mwanamke wangu.” Akasema: ”Mwambie chini yake aweke kanzu. Kwani mimi nachelea isije kuonyesha maumbo yake.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha mwanamke yule aweke kanzu chini yake ili isije kuonyesha maumbo ya mwili wake. Amri inapelekea katika uwajibu, kama inavyotambulika kwa wanazuoni. Kwa ajili hiyo ash-Shawkaaniy (02/97) amesema chini ya Hadiyth hii:

”Hadiyth inafahamisha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kufunika mwili wake wote kwa nguo isiyoonyesha maumbo yake. Hii ni sharti ya kufunika uchi. Amemwamrisha kuweka nguo chini yake kwa sababu nguo ya kikoptiki ni nguo nyembamba ambayo haifuniki ngozi kutokana na macho. Bali nguo hiyo huonyesha maumbo.”

Kama unavyoona ameifasiri Hadiyth na nguo nyembamba na inayoonyesha mwili ambayo haifichi rangi ya ngozi na kutokana na hilo ni sawa kuiweka katika sharti iliyotangulia. Lakini sioni kuwa tafsiri hiyo ni ya sawa. Hadiyth inahusiana na nguo nene inayoonyesha maumbo ya mwili ijapo sio nyembamba na iliyopwaya. Hilo liko wazi kwa njia mbili:

1 – Ameweka wazi ya kwamba nguo hiyo ya kikoptiki ilikuwa nene. Ni vipi nguo kama hiyo itafunika rangi ya ngozi na wakati huohuo iwavutie watazamaji? Pengine ash-Shawkaaniy (Rahimahu Allaah) alighafilika na kifunganishi hiki ”nene” katika Hadiyth na akafasiri Hadiyth kwa vile inavokuwa msingi wake.

2 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameweka wazi makatazo kwenye nguo hiyo na akasema:

”Kwani mimi nachelea isije kuonyesha maumbo yake.”

Kwa hivyo kilichokhofiwa ni kuonyesha maumbo, na si rangi ya ngozi.

Huenda mtu akauliza ni yepi malengo ya kanzu iliyowekwa chini ya vazi nene. Malengo ni maumbo yasionekane. Nguo nene pia zinaweza kuonyesha maumbo ya mwili wa mtu ikiwa ni zenye kubana mwili, kama zilivyo baadhi ya nguo za leo za hariri na nguo za sufu. Ndio maana Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha kuweka kanzu chini yake – na Allaah (Ta´ala) ndiye mjuzi zaidi.

[1] adh-Dwiyaa’ al-Maqdisiy katika ”al-Ahaadiyth al-Mukhtaarah” (1/441), Ahmad na al-Bayhaqiy. Inatiliwa nguvu na Dihyah mwenyewe, kama alivyopokea Abu Daawuud, al-Bayhaqiy na al-Haakim ambaye ameisahihisha Hadiyth, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa vyema. Nimeizungumzia Hadiyth hiyo kwa upambanuzi katika ”ath-Thamar al-Mustatwaab” na kwa ajili hiyo sintorejelea tena.  

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 131-133
  • Imechapishwa: 15/10/2023