78. Kumswalia Mtume, mahala pake na matamshi yake

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijiswalia mwenyewe katika Tashahhud ya kwanza na nyenginezo[1]. Amelisunisha hilo kwa Ummah wake pale alipowaamrisha kumuomba Allaah amsifu baada ya kumtakia amani[2]. Aliwafunza sampuli mbalimbali za matamshi ikiwa ni pamoja na:

اللهم صل على محمد و على أهل بيته و على أزواجه و ذريته كما صليت على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد، و بارك على محمد و على آل بيته و على أزواجه و ذريته كما باركت على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

“Ee Allaah! Msifu[3] Muhammad, jamaa zake wa nyumbani, wakeze na kizazi chake kama Ulivyowasifu jamaa zake wa nyumbani wa Ibraahiym! Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa! Na mbariki[4] Muhammad na jamaa zake wa nyumbani kwake, wakeze, kizazi chake kama Ulivyowabariki jamaa wa nyumbani wa Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa!”

Haya aliomba mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[5].

[1] Abu ´Awaanah (2/324) na an-Nasaa’iy.

[2] Walisema: “Ee Mtume wa Allaah! Tumejua ni namna gani tutavyokuombea amani (yaani katika Tashahhud), lakini vipi tutakuswalia?” Akasema: “Semeni: “Ee Allaah! Msifu Muhammad… “

Hakutofautisha Tashahhud. Ni dalili inayofahamisha kuwa ni jambo limewekwa katika Shari´ah kumswalia yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Tashahhud ya kwanza pia. Maoni hayo yuko nayo Imaam ash-Shaafi´iy, kama alivyobainisha katika “al-Umm” (01/102-105). Maoni hayo ni sahihi kwa mtazamo wa wenzake, kama alivyosema hayo wazi an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (03/460) na akasisitiza katika “ar-Rawdhwah” (01/263). Hilo pia ndio chaguo la Ibn Hubayrah al-Hanbaliy katika “al-Ifswaah”, kama alivyonukuu na kulikubali Ibn Rajab katika “Dhayl-ut-Twabaqaat” (01/280). Kuna Hadiyth nyingi zinazosema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatakiwa kuswaliwa katika Tashahhud bila upambanuo uliotajwa. Bali swalah hiyo imekuja kwa ujumla na inakusanya Tashahhud zote. Nimezitaja kama maelezo ya chini katika asili na sio kama matini kwa sababu hayatimizi masharti yangu japokuwa ni zenye kupeana nguvu inapokuja kimaana. Wale wanaopinga hawana dalili sahihi, kama nilivyopambanua katika asili. Kama ambavyo hakuna msingi wowote katika Sunnah wala hoja inayokinaisha inayosema kwamba imechukizwa kusoma katika Tashahhud ya kwanza zaidi ya:

اللهم صل على محمد

“Ee Allaah! Msifu Muhammad… “

Naona kwamba anayesema hivi pekee basi hafuamti maamrisho ya hapo nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

اللهم صل على محمد و على آل محمد

“Ee Allaah! Msifu Muhammad na jamaa zake wa nyumbani… “

Nimetaja maudhui yote katika asili.

[3] Maneno bora yaliyosemwa ni yale ya Abul-´Aaliyah:

“Maana ya Allaah kumswalia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kumsifu na kumuadhimisha. Malaika na wengineo kumswalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kule kumuomba Allaah amsifu. Makusudio ni kule kuomba asifiwe kwa kuzidishiwa.”

Haafidhw Ibn Hajar ametaja katika “Fath-ul-Baariy” na akaraddi maoni yanayomaanisha kwamba Mola kumswalia manaa yake ni rehema. Ibn-ul-Qayyim amefafanua vya kutosha kwa undani kabisa katika ”Jalaa’-ul-Afhaam”. Rejea huko!

[4] Baraka ni ukuaji na kuongezewa. Katika du´aa hii anaombwa Allaah ampe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kheri Alizowapa jamaa zake Ibraahiym, kumdumisha nazo na kumzidishia zaidi na zaidi.

[5] Ahmad na at-Tahaawiy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Kadhalika ameipokea al-Bukhaariy na Muslim pasi na neno “jamaa zake”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 143-144
  • Imechapishwa: 01/01/2019