Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah ni kusadikisha karama za mawalii na yale matukio yasiyokuwa ya kawaida ambayo Allaah hufanya yakapitia kwao, ima katika aina mbalimbali za elimu na maono, uwezo maalum na taathira. Vilevile yale yaliyopokelewa kuhusu watu waliotangulia katika Suurah “al-Kahf” na mengineyo, na vivyo hivyo kuhusu watu waliotangulia katika ummah huu miongoni mwa Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na watu wa ummah zingine zilizobaki, nayo yataendelea kuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.
MAELEZO
Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, ni kama alivyosema mtunzi wa kitabu ambaye ni Abul-´Abbaas Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah), ni kusadikisha karama za mawalii zilizotajwa ndani Qur-aan na Sunnah na yaliyopitika baada ya hapo.
Karama ni kitu kinachofanywa na mtu kisichokuwa cha kawaida. Ni kitu kisichokuwa cha kawaida kwa viumbe wengine. Haya yanaitwa kuwa ni “karama” pale yanapofanywa na mtu miongoni mwa mawalii wa Allaah wakweli. Endapo mambo kama haya yatafanywa na wasiokuwa wao itakuwa ni uchawi na mambo ya kishaytwaan. Tofauti na yakifanywa kupitia mtu ambaye ni muumini inakuwa ni karama za mawalii.
Haitokuwa karama isipokuwa mpaka pale itapojulikana kuwa mtu amenyooka sawa katika dini ya Allaah, kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah):
“Lau ataruka angani au akapita juu ya maji hazingatiwi kuwa ni walii.”
Ni lazima apimwe kwa mizani ya Qur-aan na Sunnah. Akiwa amenyooka juu ya Qur-aan na Sunnah huyo ndiye walii wa Allaah. Vinginevyo atakuwa ni katika mawalii wa shaytwaan. Amesema (´Azza wa Jall):
إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ
“Hawakuwa mawalii Wake isipokuwa wale wenye kumcha.” (08:34)
أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ
“Zindukeni! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika, ambao wameamini na wakawa wanamcha Allaah.” (10:62-63)
Miongoni mwao ni pamoja vilevile na watu wa pangoni. Allaah aliwakirimu kusinzia [ndani ya pango] kwa miaka 309. Baada ya hapo Allaah akawahuisha. Hii ni ishara miongoni mwa ishara za Allaah kutokana na imani na kumcha kwao Allaah. Allaah aliwafanya kuwa ni alama na mazingatio.
Kadhalika kama ilivyopitika kwa ´Abbaad bin Bishr na Usayd bin Hudhwayr (Radhiya Allaahu ´anhum). Usiku mmoja wenye giza walikuwa wametoka nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ghafla kila mmoja katika wao bakora yake ikamwangazia taa mpaka walipofika majumbani mwao.
Vilevile kisa cha at-Twufayl ad-Dawsiy (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipoingia katika Uislamu watu wake walichelewa kusilimu. Ndipo akamwambia Mtume wa Allaah amuombee kwa Allaah amfanye awe na alama huenda wakaongoka. Akamuombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Allaah amfanye kuwa na alama ili awaongoze kwayo watu wake. Allaah akafanya kati ya macho yake akawa na kitu mfano wa taa pale anapowaendea watu wake. Akamuomba Mola Wake aliweke kwengine mbali na uso. Ndipo Allaah akaiweka nuru hiyo kwenye fimbo yake; kila anapoinyanyua bakora yake inaangaza. Allaah akawaongoza kwayo watu wake kupitia kwake na akawafanya kuwa waislamu[1].
Makusudio ni kwamba ni mambo yanayoenda kinyume na mazowea. Ikiwa mwenye kuyafanya ni mtu anayemcha Allaah na anatambulika kwa wema, basi ayafanyayo ni karama. Na ikiwa ni kinyume na hivyo, basi ayafanyayo ni katika mambo ya wachawi na ya kishaytwaan.
[1] Abu Nu´aym katika ”Ma´rifat-us-Swahaabah” (3500) na al-Bayhaqiy katika ”Dalaa-il-un-Nubuwwah” (2108).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 120-121
- Imechapishwa: 03/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)