44. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya karama za mawalii

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah ni:

Kusadikisha karama za mawalii na yale matukio yasiyokuwa ya kawaida ambayo Allaah Hufanya yakapitia kwao, ima katika aina mbali mbali za elimu, maono, uwezo maalum na taathira, na yaliyopokelewa kuhusu watu waliotangulia katika Suurah “al-Kahf” na kadhalika. Hali kadhalika kuhusu watu waliotangulia katika Ummah huu miongoni mwa Maswahabah, Taabi´uun na watu wa Ummah zingine zilizobaki, nayo yataendelea kuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.

Katika njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni:

Kufuata mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa undani na kwa uinje, na kufuata njia ya waliotangulia katika Muhaajiruun na Answaar, na kufuata wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi aliposema:

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo bara bara na ziumeni kwa magego yenu. Na tahadharini na mambo ya yakuzua! Kwani hakika kila Bid´ah ni upotevu.”

Na wanajua ya kwamba hakika maneno ya kweli kabisa, ni Maneno ya Allaah, na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanayapa kipaumbele Maneno ya Allaah yatangulie mbele kabla ya maoni ya watu wengine na wanatanguliza uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya uongofu wa wengine wote. Na kwa ajili hii ndio wakaitwa “Ahl-ul-Kitaab was-Sunnah”. Wanaitwa vilevile Ahl-ul-Jamaa´ah” kwa kuwa “Jamaa´ah” ni ile iliokusanyika. Na kinyume chake ni “al-Furqah”[1], hata kama lafdhi ya “al-Jamaa´ah” imekuwa ni jina la watu wote waliokusanyika.

Ijmaa´ ndio msingi wa tatu unaotegemewa katika elimu na dini. Nao Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanapima kwa misingi hii mitatu mambo yote ya dini kuhusiana na maneno na matendo ya watu, sawa yaliyojificha na yaliyodhahiri. Ijmaa´ ni yale waliokubaliana Salaf as-Swaalih, kwa kuwa baada yao kulikithiri tofauti na Ummah ukagawanyika.

MAELEZO

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah… – Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, ni kama alivyosema mwandishi ambaye ni Abul-´Abbaas Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah), ni kusadikisha karama za mawalii, aliyotaja Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu yao na yaliyopitika baada ya hapo.

Karama ni kitu kinachofanywa na mtu kisichokuwa cha kawaida. Ni kitu kisichokuwa cha kawaida kwa viumbe wengine. Haya yanaitwa kuwa ni “karama” pale yanapofanywa na mtu miongoni mwa mawalii wa Allaah wakweli. Endapo mambo kama haya yatafanywa na wasiokuwa wao – yaani waumini wakweli – itakuwa ni uchawi na mambo ya mashaytwaan. Tofauti na yakifanywa kupitia mtu ambaye ni muumini inakuwa ni karama za mawalii.

Haitokuwa karama isipokuwa mpaka pale itapojulikana kuwa mtu amenyooka katika dini ya Allaah, kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah):

“Lau ataruka angani au akapita juu ya maji hazingatiwi kuwa ni walii.”[2]

Ni lazima apimwe kwa mizani ya Qur-aan na Sunnah. Akiwa amenyooka juu ya Qur-aan na Sunnah huyo ndiye walii wa Allaah. Vinginevyo atakuwa ni katika mawalii wa shaytwaan. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ ۚ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ

“Na hawakuwa ni mawalii Wake. Hawakuwa mawalii Wake isipokuwa wenye taqwa.” (08:34)

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wana taqwa.” (10:62-63)

Miongoni mwao ni pamoja vilevile na watu wa al-Kahf. Allaah aliwakirimu kusinzia [ndani ya pango] kwa miaka mia tatu na wakazidisha tisa. Baada ya hapo Allaah akawahuisha. Hii ni ishara miongoni mwa ishara za Allaah kutokana na imani na taqwa yao. Allaah aliwafanya kuwa ni alama na funzo.

Kadhalika kama ilivyopitika kwa ´Abbaad bin Bishr na Usayyid bin Hudhwayr ambao ni Maswahabah wawili watukufu waliokuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wametoka nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika usiku wenye giza. Ghafla kila mmoja akaangaziwa katikati yake taa lenye kumwangazia njia mpaka kila mmoja alipofika nyumbani kwa familia yake[3].

Vilevile kisa cha at-Twufayl ad-Dawsiy, ambaye alikuwa ni mkuu wa kabila la Daws, pindi alipoingia katika Uislamu watu wake walichelewa kusilimu. Ndipo akamwambia Mtume wa Allaah amuombee kwa Allaah amfanye awe na alama huenda wakaongoka. Akamuombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Allaah amfanye kuwa na alama ili awaongoze kwayo watu wake. Allaah akafanya kati ya macho yake akawa na kitu mfano wa taa pale anapowaendea watu wake. Akamuomba Mola Wake aliweke kwengine mbali na uso. Ndipo Allaah akaiweka nuru hiyo [nuru] kwenye sauti yake pale anapozungumza. Allaah akawaongoza kwayo watu wake kupitia kwake na akawafanya kuwa waislamu[4].

Makusudio ni kwamba ni mambo yanayoenda kinyume na mazowea. Ikiwa mwenye kuyafanya ni mtu anayemcha Allaah na anatambulika kwa wema, basi ayafanyayo ni karama. Na ikiwa ni kinyume na hivyo, basi ayafanyayo ni katika mambo ya wachawi na mashaytwaan. Kwa haya [karama wazifanyazo mawalii] ni kwa sababu ya kufuata kwao Qur-aan na Sunnah.

Qur-aan, Sunnah kwa ufahamu wa Salaf

Katika njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kufuata mapokezi… – Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah ni kufuata mapokezi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale waliyokuwemo makhaliyfah waongofu. Huu ni mwenendo mmoja wapo wa Ahl-us-Sunnah. Wanafuata mfumo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mapokezi yake na mapokezi ya makhaliyfah wake waongofu. Hii ndio njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kwa ajili hii ndio maana wanaitwa “Ahl-ul-Kitaab was-Sunnah”, “Ahl-ul-Jamaa´ah”. Neno “Jamaa´ah” ni mkusanyiko na kinyume chake ni al-Furqah. Wameitwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa sababu wamekusanyika katika Kitabu na Sunnah, wakayasadikisha na wakayapima mambo yao kwavyo. Hawa ndio Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wamekusanyika katika kuiadhimisha Qur-aan na Sunnah na kuvitendea kazi. Kwa misingi hii mitatu wanayapima maneno na vitendo vyote vya watu.

Msingi wa kwanza ni Qur-aan.

Msingi wa pili ni Sunnah Swahiyh.

Msingi wa tatu ni Ijmaa´ yenye kudhibitiwa. Inahusiana na yale maafikiano ya Salaf ambayo ni ya Maswahabah Radhiya Allaahu ´anhum). Maneno na vitendo vyote vinavyofanywa na watu vinapimwa na misingi hii. Yanayoafikiana navyo yanakubaliwa na yanayoenda kinyume navyo anarudishiwa mwenye nayo. Pasi na kujali atakuwa nani.

[1] Mgawanyiko.

[2] Tazama “al-Furqaan baina Awliyaa´-ir-Rahmaan wa Awliyaa´-ish-Shaytwaan”, uk. 45.

[3] Tazama Fataawaa za Shaykh “Nuur ´alaad-Darb” (02/191-193).

[4] Abuu Na´iym al-Aswbahaaniy katika “Ma´arifat-us-Swahaabah” (11/175) (3500) na al-Bayhaqiy katika “ad-Dalaail-un-Nubuwwah (05/460) (2108).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com