77. Sharti ya kwanza inayomfunguza mfungaji: Utambuzi

Ndugu wapendwa! Hakika vifunguzi vilivyotangulia – mbali na hedhi na nifasi – navyo ni jimaa, kutokwa na manii kwa kuchanganyika na wanawake, kula, kunywa na vilivyo na maana ya viwili hivyo, kuumikwa na kujitapisha. Hakuna chochote katika vitu hivyo kinachomfunguza mfungaji isipokuwa akivitumia kwa kujua, kwa kukumbuka na kwa kutaka kwake mwenyewe. Ni lazima yapatikane masharti haya matatu:

1 – Awe mtambuzi. Akiwa mjinga hakumfunguzi. Amesema (Ta´ala) katika Suurah “al-Baqarah”:

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[1]

Allaah akasema:

“Nimekwishafanya.”[2]

Amesema tena (Ta´ala):

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini [itakuwa dhambi] katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu; na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[3]

Ni mamoja mtu huyo ni mjinga kuhusu hukumu ya ki-Shari´ah. Kwa mfano akadhani kuwa kitu hicho si chenye kufunguza ambapo akakifanya, au hajui hali na wakati. Kwa mfano akadhani kuwa alfajiri haijachomoza ambapo akala ilihali kumekwishapambazuka, au akadhani kuwa jua limekwishazama ambapo akala ilihali bado halijazama. Hali zote hizo hazimfunguzi. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“… mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi.”[4]

Nikategemea nyuzi mbili; moja ilikuwa nyeusi na nyingine ilikuwa nyeupe ambapo nikaziweka chini ya mito yangu na nikawa naziangalia. Wakati ulipobainika uzi mweupe kutokamana na mweusi nikajizuia na kula na kunywa. Wakati asubuhi ilipofika nikaenda mapema kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza nilichokifanya. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ikiwa uzi mweusi na mweupe. Hivyo mto wako basi hakika utakuwa mpana. Hakika hapana vinginevyo hilo ni weupe wa mchana na weusi wa usiku.”

Hivyo ´Adiyy akaendelea kula baada ya kuingia kwa alfajiri na hakujizuia kula mpaka alipobainikiwa na nyuzi mbili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumwamrisha kulipa kwa sababu alikuwa hajui hukumu. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Siku moja ambapo mawingu yalikuwa yametinga tulikata swawm katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya muda jua likachomoza.”

Hakutaja kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaamrisha kulipa kwa sababu walikuwa hawajui wakati. Endapo wangeamrishwa kulipa basi ingenakiliwa. Kwa sababu kuna kila sababu inayopelekea kulinukuu kutokana na umuhimu wake. Bali Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake “Haqiyqat-us-Swiyaam”:

“Hishaam bin ´Urwah, ambaye ni mmoja wa wapokezi wa Hadiyth, amepokea kutoka kwa baba yake ´Urwah ya kwamba hawakuamrishwa kulipa.”

Lakini pale tu ambapo watu watajua kuwa bado ni mchana na kwamba jua halijazama basi watajizuia na kula na kunywa mpaka lizame.

Mfano wa hilo ni kama mtu atakula baada ya kuchomoza kwa alfajiri na wakati huohuo akidhani kuwa haijachomoza, lakini baadaye ikambainikia kuwa imekwishachomoza, basi swawm yake ni sahihi na halazimiki kulipa kwa sababu alikuwa mjinga wa wakati. Allaah amemruhusu kula, kunywa na kufanya jimaa mpaka abainikiwe na alfajiri. Mtu aliyefanya jambo lililoruhusiwa na kuidhinishwa haamrishwi kulilipa. Lakini pindi itampobainikia wakati yuko anakula na kunywa ya kwamba jua halijazama au alfajiri imekwishachomoza, basi atajizuia na kutema kile kilichomo ndani ya mdomo wake akiwa na kitu. Kwa sababu kipindi hicho udhuru wake utakuwa umeondoka.

[1] 02:286

[2] Ameipokea Muslim.

[3] 33:05

[4] 02:187

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 105-107
  • Imechapishwa: 01/03/2024