Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Wanawapenda na kufanya urafiki na watu wa familia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanachunga wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu yao aliposema siku ya Ghadiyr Khumm:

“Na watu wa nyumba yangu. Ninawakumbusha kwa Allaah kuhusiana na watu wa nyumbani kwangu. Ninawakumbusha kwa Allaah kuhusiana na watu wa nyumbani kwangu.”[1]

Vilevile alimwambia ami yake al-´Abbaas ambaye alikuwa amekuja kushtaki ya kwamba baadhi ya Quraysh wanawachukia wana wa Haashim:

“Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Hawatoamini mpaka wawapende kwa ajili ya Allaah na kwa ukaribu wenu kwangu.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tena:

“Allaah amewachagua wana wa Ismaa´iyl. Na  kutoka wana wa Ismaa´iyl amechagua Kanaanah. Na kutoka Kanaanah amechagua Quraysh. Na kutoka Quraysh amechagua wana wa Haashim na amenichagua mimi kutoka Banuu Haashim.”[3]

Vivyo hivyo wanawapenda na kufanya urafiki na wakeze Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao ndio mama wa waumini, na wanaamini ya kwamba wao ndio wakeze Aakhirah, na khaswakhaswa Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ndiye mama wa watoto wake wengi. Jengine ni kwamba yeye ndiye alikuwa wa kwanza kumwamini na kumsaidia juu ya kazi yake. Alikuwa ni mwenye nafasi ya juu kwake. Mambo ni vivyo hivyo kuhusu yule mwanamke mkweli mno, msichana wa yule bwana ambaye ni mkweli mno, ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Ubora wa ´Aaishah kwa kulinganisha na wanawake wengine ni kama ubora wa uji kulinganisha na chakula chengeni.”[4]

Wanajitenga mbali na njia ya Raafidhwah ambao wanawachukia na kuwatukana Maswahabah. Wanajitenga mbali na Nawaaswib ambao wanawaudhi watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) eitha kwa maneno au matendo.

Wanayanyamazia yale yaliyopitika kati ya Maswahabah. Wanasema kwamba haya mapokezi yaliyopokelewa kuna ambayo ni ya uwongo, kuna ambayo yamezidishwa juu yake, mengine yamepunguzwa, mengine yamebadilishwa kinyume na sura yake ya kihakika na mengine ambayo ni sahihi ambayo walikuwa ni wenye kujitahidi na wakapatia au walikuwa ni wenye kujitahidi na wakakosea.

Wao pamoja na hivyo hawaitakidi ya kwamba kila mmoja katika Maswahabah amekingwa na dhambi kubwa au ndogo. Bali kinyume chake kuna uwezekano wakafanya dhambi kwa ujumla. Kule kutangulia kwao awali na fadhilah walizonazo zinafanya wao kusamehewa kwa yale makosa ambayo yanaweza kutokea kwao. Wanaweza hata kusamehewa kwa yale madhambi ambayo yasingelisamehewa kwa mwengine yeyote baada yao, kwa sababu wanayo mema mengi ambayo hana yeyote aliyekuja baada yao. Kumethibiti kwa maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba wao ndio kizazi bora[5] na kwamba akitoa swadaqah mmoja wao kiasi cha kibaba ina uzito zaidi kuliko inayotolewa na aliyekuja baada yao, hata kama huyu atatoa dhahabu sawa na kiasi cha mlima wa Uhud. Ikiwa mmoja wao atapitikiwa na dhambi, atakuwa ima ametubia kwa dhambi hiyo, au alifanya mema ambayo yameifuta au amesamehewa kwa fadhilah za kutangulia kwake awali, au [kasamehewa] kwa uombezi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao hakuna ambaye ana haki zaidi ya uombezi wake isipokuwa wao au alipewa mtihani kwa majaribio ya duniani ambayo yamefuta dhambi yake hiyo. Ikiwa mambo ni namna hii kwa yale madhambi yaliyothibiti, kusemwe nini juu ya yale mambo ambayo walikuwa wenye kujitahidi katika kuifikia haki? Ikiwa wamepatia wana ujira mara mbili, na wakikosea wana ujira mara moja na kosa lao limesamehewa. Isitoshe madhambi ambayo yanaweza kuwa yalitokea kwa baadhi yao ni machache mno na ni yenye kusamehewa ukilinganisha na fadhilah za nafasi yao na mema yao, kama vile kumwamini Allaah na Mtume Wake, kupigana jihaad katika njia ya Allaah, kuhajiri, nusura, elimu yenye manufaa na matendo mema.

Yule atakayetazana historia ya Maswahabah kwa elimu na umaizi na zile fadhilah alizowaneemesha Allaah kwazo, basi atatambua kwa yakini ya kwamba wao ndio viumbe bora kabisa baada ya Mitume. Kamwe hakupatapo kuwepo na hakutokuwepo mtu mfano wao. Wao ndio wasomi wa wasomi katika ummah huu ambao ndio watu bora na watukufu zaidi mbele Allaah (Ta´ala).

MAELEZO

Ni wajibu kwa watu wa imani baada yao kufuata mfumo wao na waamini kuwa Maswahabah wote ndio wabora wa ummah na wenye fadhilah zaidi. Kuhusiana na kasoro zenye kusimuliwa kutoka kwa baadhi ya Maswahabah ni chache sana ukilinganisha na kheri nyingi alizowapa Allaah, fadhilah zao na matendo yao makubwa. Aliyofanya mmoja wao ima atakuwa alitubia kwayo, alifanya jema lililofuta ovu hilo, alisamehewa na fadhilah za kutangulia kwake, atapata uombezi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kwani wao ni wenye haki zaidi ya kupata uombezi wake – au kwa sababu ya mitihani ya maradhi na mengineyo ambayo yalifanya akasamehewa.

Hivi ndivyo wanavyoonelea Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika masuala haya yaliyotajwa na mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah). Muumini anatakiwa kuuhifadhi mlango huu vizuri na atendee kazi maana yake. Vilevile ´Aqiydah yake inatakiwa iwe imebobea ili aweze kutofautiana na Ahl-ul-Bid´ah wote ikiwa ni pamoja na Raafidhwah, Nawaaswib na wengineo. Raafidhwah wamechupa mipaka kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), upande mwingine Khawaarij, Mu´tazilah na mfano wao wanazembea juu ya haki za Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wa familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunamuomba Allaah awawie radhi na atujaalie kuwa ni miongoni mwa wenye kuwafuata kwa wema.

[1] Muslim (2408).

[2] Ahmad (1/207).

[3] Muslim (2276).

[4] al-Bukhaariy (3411) na Muslim (2431).

[5] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2535).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 117-118
  • Imechapishwa: 03/11/2024