Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Wanamshuhudilia Pepo yule ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemshuhudilia, kama wale kumi, na Thaabit bin Qays bin Shimmaas na Maswahabah wengineo. Na wanayathibitisha yale yaliyopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhu) na wengineo, ya kwamba mbora wa ummah huu baada ya Mtume wake ni Abu Bakr na kisha ´Umar. Wanaona kuwa ´Uthmaan anakuja nafasi ya tatu na ´Aliy anakuja nafasi ya nne, kama yalivyofahamisha masimulizi. Hali kadhalika kama jinsi Maswahabah walivyoafikiana kumtanguliza mbele ´Uthmaan kwa kumpa kiapo cha utiifu, ingawa wapo baadhi ya Ahl-us-Sunnah waliotofautiana juu ya ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) – baada ya kuafikiana kwao kumtanguliza mbele Abu Bakr na ´Umar – ni nani aliyebora. Kuna baadhi ambao wamemtanguliza ´Uthmaan kisha baada ya hapo wakanyamaza au wakasema kuwa wanne ni ´Aliy. Na baadhi ya wengine wakamtanguliza ´Aliy na wengine wakasimama.
Lakini mwishoni Ahl-us-Sunnah wakaafikiana kumtanguliza ´Uthmaan kisha ´Aliy, ijapo suala hili – kuhusu nani bora kati ya ´Uthmaan na ´Aliy – wengi katika Ahl-us-Sunnah wanaona kuwa sio ya msingi ambayo atatiwa upotofuni yule atakayeyakhalifu, lakini masuala ambayo mtu atahukumiwa upotevu ni masuala ya ukhaliyfah. Hili ni kwa sababu wanaamini ya kwamba Khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan na kisha ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Atayakekashifu uongozi wa mmoja katika hawa, basi ni mpotevu kuliko punda wa kufugwa.
MAELEZO
Kadhalika wanamshuhudilia yule ambaye ameshuhudiliwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Pepo ikiwa ni pamoja na wale Maswahabah kumi, Thaabit bin Qays bin Shammaas, ´Abdullaah bin Salaam, ´Ukkaashah bin Mihswan na wengineo ambao wameshuhudiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanatakiwa kushuhudiliwa. Ambaye kumethibiti kushuhudiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anashuhudiliwa.
Vivyo hivyo wanaamini yaliyothibiti kuhusu watu wa vita vya Badr ambapo waliambiwa:
“Fanyeni mtakacho, kwani Nimeshawasameheni.”
Vilevile wanaamini kuwa hatoingia Motoni yeyote ambaye alitoa kiapo cha utiifu chini ya mti. Hiki ni kile kiapo cha Ridhwaan. Kwa sababu imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:
“Hakuna yeyote kati yenu aliyekula kiapo cha utiifu chini ya mti atakayeingia Motoni.”
Sivyo tu, bali Allaah akateremsha kuhusu wao:
لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا
”Hakika Allaah amewawia radhi waumini waliokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti [Allaah] alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao, basi akawateremshia utulivu na akawalipa ushindi wa karibu.” (48:18)
Yote haya ni katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 116-117
- Imechapishwa: 03/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)