76. Athar ”Hakika baadhi ya watu wanapambana kuitafuta dunia… ”

76 – Abu Bakr bin Abiy Shaybah ametuhadithia: Husayn bin ´Aliy ametuhadithia, kutoka kwa Ja´far bin Burqaan, ambaye amesimulia kuwa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz aliandika:

”Hakika baadhi ya watu wanapambana kuitafuta dunia kwa matendo ya Aakhirah. Baadhi ya wapiga visa wamezua du´aa ya kuwaswalia makhalifah na viongozi wao badala ya kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati itapokufikia barua yangu hii, basi waamrishe du´aa zao ziwe kuwaswalia Mitume, kuwaombea du´aa waislamu kwa jumla na wayaache mengine yasiyokuwa hayo.”[1]

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh na yenye kukatika. Husayn bin ´Aliy ni Ibn-ul-Waliyd al-Ju´fiy. Imaam Ibn-ul-Jawziy ameitaja barua hii katika kitabu chake “´Umar bin ´Abdil-´Aziyz”. Iko namna hii kwa utimilifu wake:

”Kutoka kwa ´Umar, mja na Kiongozi wa waumini, kwenda kwa makamanda wa askari.

Muda wa kuwa watu wanafuata Kitabu cha Allaah, basi watanufaika katika dini, maisha yao ya dunia na marejeo kwa Allaah baada ya kufa. Hakika Allaah ameamrisha ndani ya Kitabu chake kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Mtume. Hivyo enyi walioamini mswalieni na mumsalimu kwa salamu.” (33:56)

Allaah amsifu na kumsalimisha Mtume Wake Muhammad, amrehemu na ambariki!

Kisha akasema kumwambia Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ

”… na omba msamaha kwa dhambi zako na kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike. Allaah anajua harakati zenu huku na kule na pahala penu pa kupumzikia.” (47:19)

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ndani ya Kitabu Chake amekusanya kati ya kuamrisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini wa kiume na  waumini wa kike. Baadhi ya wapiga visa wamezua du´aa ya kuwaswalia makhalifah na viongozi wao badala ya kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini.  Wakati itapokufikia barua yangu hii, basi waamrishe wapiga visa wenu kuwaswalia Mitume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika nyuradi na du´aa zao, kisha wawaswalie waumini wa kiume na waumini wa kike. Halafu waombe nusura kutoka kwa Allaah. Maombi yao yawe ya jumla kwa waislamu na wayaache mengine yasiyokuwa hayo. Tunamuomba Allaah mawafikisho katika mambo yote, uwongofu, usawa na mwongozo katika anayoyapenda na kuyaridhia. Hapana uwezo wa kutikisika wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah, Aliye juu kabisa, Mkuu. Amani ya Allaah iwe juu yako.”

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Ishaaq al-Maalikiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-us-Swalaah ´alaan-Nabiy, uk. 69-71
  • Imechapishwa: 05/02/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy