Swali 75: Kwa sababu ya matukio fulani wamekuwepo waislamu wanaowapenda makafiri kwa sababu ya fatwa waliyosikia kutoka kwa mmoja katika wanafunzi. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Sidhani kama kuna muislamu anayewapenda makafiri. Lakini nyinyi mnafasiri mapenzi kwa isiyokuwa maana yake. Ikiwa anawapenda kikweli, basi huyo ima ni mjinga au sio muislamu bali ni katika wanafiki. Kuhusu muislamu hawapendi makafiri. Lakini yako matendo ambayo mnafikiria kuwa ni mapenzi ilihali sivyo, kwa mfano kufanya biashara na makafiri, kuwapa zawadi makafiri na kukubali zawadi kutoka kwa makafiri. Haya yanafaa na sio katika mapenzi. Haya ni miongoni mwa miamala ya kidunia na kubadilishana manufaa. Mfano mwingine ni muislamu kumwajiri kafiri amfanyie kazi sio mapenzi – ni katika kubadilishana manufaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuajiri ´Abdullaah bin Urayqitw al-Laythiy ili amwongoze njia kutoka Makkah kwenda Madiynah wakati alipohajiri. Bwana huyo alikuwa kafiri na alikuwa anaijua njia vizuri.

Inafaa pia kwa muislamu kufanya kazi kwa makafiri akihitaji. Hili pia ni katika kubadilishana manufaa. Haihusiani na kuwapenda na kujenga urafiki, bali ni kulipiza wema kwa wema. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ

“Hutopata watu wanaomuamini Allaah na siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake, japo wakiwa ni baba zao, watoto wao, ndugu zao au jamaa zao.”[1]

Lakini wanatakiwa kutendewa wema. Kwa sababu kufanya hivo ni katika wema wa kidunia na kumrudishia wema baba.

Wakati mwingine kunakuwepo suluhu na mapatano ya amani na makafiri. Haya sio mapenzi. Yapo mambo ambayo baadhi ya wajinga wanafikiria kuwa ni mapenzi ilihali mambo sivyo[2].

Wakati mwingine waislamu wanakuwa khatarini na wakawapa kitu cha kidunia makafiri ili kuepuka shari yao. Haya sio mapenzi. Wala sio kujikombakomba kwao. Kuwapa kitu cha kidunia kunatofauti na kujikombakomba. Kujikombakomba haijuzu. Kuwapa kitu cha kidunia inajuzu. Mambo haya yanahitaji kueleweka na kutambulika. Ama kufasiri kila kitendo na makafiri kwamba ni kuwapenda ni ujinga na makosa. Au ni kuwababaisha watu.

Kwa kufupisha ni kwamba hakuna anayetakiwa kuingia ndani ya mambo haya isipokuwa wanazuoni peke yake. Si jambo la wanafunzi. Hawatakiwi kujiingiza katika mambo hayo, wakahalalisha, wakaharamisha na wakawatuhumu watu hili na lile. Wanayaita mambo kuwa ni mapenzi ilihali hawajui hukumu kwa mujibu wa Shari´ah. Mzungumzaji anajiweka ndani ya khatari kwa sababu anazungumza juu ya Allaah pasi na elimu[3].

[1] 58:22

[2] Wako wapi wale ambao wamejiteu wenyewe kuwa walinganizi, waelekezaji na viongozi juu ya Sunnah hii kuhusiana na kufanya biashara na makafiri? Ima ni wajinga. Katika hali hiyo wanalazimika kusoma kabla kuongoza. Au wakawa na elimu juu ya hilo. Katika hali hiyo wanatakiwa kumcha Allaah na wawabainishie watu haki na wasifuate matamanio.

[3] Kuongea juu ya Allaah pasi na elimu ni jambo la khatari na dhambi kubwa zaidi kuliko shirki. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika si vyenginevyo Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.” (7:33)

Kinacholengwa ni kuwa ukhatari wa madhambi umeongezeka kwa mpangilio. Kuzungumza juu ya Allaah bila ya elimu ni khatari zaidi kuliko shirki kwa sababu yule mzungumzaji ameweka mwekaji Shari´ah na si mwenza peke yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 191-193
  • Imechapishwa: 14/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy