Madaftari (الدواوين) ni wingi wa daftari. Kusambazwa maana yake kilugha ni daftari ambalo hudhibitiwa wanajeshi na mfano wao. Madaftari maana yake katika Shari´ah ni madaftari ambayo hudhibitiwa matendo ambayo yameandikwa na Malaika kwa yule mwenye kuyatenda. Kuyatawanya na kuyagawanya madaftari ni kule kuyadhihirisha madaftari ya matendo siku ya Qiyaamah ambapo yatatawanywa kwenda mikono ya kulia na mikono ya kushoto. Ni kitu kimethibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Ummah. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًاوَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِفَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًاوَيَصْلَىٰ سَعِيرًا

”Ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, basi atahesabiwa hesabu nyepesi na atageuka kwa ahli zake hali ya kuwa ni mwenye furaha. Na ama yule atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake, basi ataomba maangamizi na ataingia aungue Moto uwakao.”[1]

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ

“Ama yule atakayepewa kitabu chake kushotoni mwake, atasema: “Ee! Laiti nisingepewa kitabu changu.”[2]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, utaikumbuka familia yako?” Akasema: “Kuhusu maeneo matatu hakuna yeyote atakayemkumbuka yeyote; katika mizani mpaka ajue mizani yake ni nyepesi au nzito, wakati wa kugawanywa madaftari mpaka ajue ni wapi kitaangukia kitabu chake kwenye mkono wa kuliani mwake au kushotoni mwake au nyuma ya mgongo wake, wakati wa Njia itapowekwa juu ya mgongo wa Moto mpaka avuke.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud na al-Haakim ambaye amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti zao wawili.”

Waislamu wameafikiana juu ya kuthibiti kwake.

[1] 84:07-12

[2] 69:25

[3] Abu Daawuud (4755), al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (04/578), al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah” (385). Ameitaja Shaykh al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Abiy Daawuud.”

al-Haakim amesema:

”Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya masharti ya Mashaykh wawili kama isingelikuwa kunyanyuliwa kwake kati ya al-Hasan na ´Aaishah.” na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

Hadiyth hiyo ina njia nyingine iliyopokelewa na Ahmad (06/110) kupitia kwa Ibn Lahiy´ah, kutoka kwa Khaalid bin Abiy ´Imraan, kutoka kwa al-Qaasim, kutoka kwa ´Aaishah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 122
  • Imechapishwa: 30/11/2022