74. Mizani ni mingapi na ni kitu gani kinachopimwa?

Wanazuoni wametofautiana; je, mzani ni mmoja au ni mingi? Baadhi wamesema kuwa ni mingi kwa kutegemea nyumati, mmojammoja au matendo. Kwa sababu haikutajwa ndani ya Qur-aan isipokuwa kwa njia ya wingi. Kuhusu kutajwa kwake kwa njia ya umoja katika Hadiyth ni kwa kuzingatia aina. Wengine wakasema kuwa ni mzani mmoja. Kwa sababu imepokelewa katika Hadiyth kwa njia ya umoja. Kuhusu kutajwa kwake kwa wingi ni kwa kuzingatia vile vitavyopimwa. Maoni yote mawili ni yenye kuwezekana na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Kitachopimwa ni matendo kutokana na udhahiri wa Aayah iliyotangulia na Hadiyth baada yake. Maoni mengine yanasema kuwa madaftari ya vitendo ndio yatapimwa kutokana na Hadiyth ya bwana yule mwenye kadi. Kuna maoni vilevile yanayosema kuwa mtendaji ndiye atapimwa kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika siku ya Qiyaamah ataletwa mtu mkubwa na mnene na hatokuwa na uzito mbele ya Allaah sawa na ubawa wa mbu.” Akasema: “Someni:

فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا

“Hatutowasimamishia siku ya Qiyaamah uzito wowote.”[1][2]

Kuna maafikiano juu yake.

Baadhi ya wanazuoni wameoanisha kati ya maandiko haya ya kwamba vyote hivyo vitapimwa au ukweli wa kitachopimwa ni yale madaftari. Kutokana na kwamba madaftari hayo yatakuwa mazito au mepesi kwa mujibu wa matendo yaliyoandikwa, ndio maana ni kana kwamba kinachopimwa ni yale matendo. Kuhusu kupimwa kwa yule mtu mwenye matendo kinachokusudiwa ni kiasi na heshima yake. Huku ni kukusanya kuzuri. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] 18:105

[2] al-Bukhaariy (4729) na Muslim (2785, 18).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 121
  • Imechapishwa: 30/11/2022