Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

63 – Matokeo yake anakuwa mwenye kuyumbayumba kati ya ukafiri na imani, kusadikisha na kukadhibisha, kutambua na kukanusha.

MAELEZO

Yule asiyejisalimisha kwa Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atakoseshwa utambuzi juu ya Allaah na kuitambua haki. Hivyo anakuwa upotofuni. Hii ndio hali ya wanafiki ambao wanakuwa wenye kuyumbayumba; mara wanakuwa pamoja na waislamu na mara wanakuwa pamoja na wanafiki. Mara wanasadikisha, mara wanakadhibisha:

كُلَّمَا أَضَاءَ لَهُم مَّشَوْا فِيهِ وَإِذَا أَظْلَمَ عَلَيْهِمْ قَامُوا

“Kila unapowaangazia njia, basi hutembea humo; na unapowafanyia kiza, basi husimama.”[1]

Kuhusu waumini husema kile wanachokijua. Yale wasiyoyajua huegemeza ujuzi wake kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) na wala hawajikakami kitu wasichokijua au wakasema juu ya Allaah yale wasiyoyajua. Kuzungumza juu ya Allaah pasi na elimu ni khatari zaidi kuliko shirki:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika si vyenginevyo Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[2]

Akafanya kumsemea Allaah pasi na elimu ni zaidi ya kumshirikisha Allaah, kitu ambacho kinajulisha ukhatari wa jambo hilo.

[1] 2:20

[2] 7:33

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 23/01/2023