Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

62 – Yule mwenye kujipinda kuyajua yale asiyokuwa na elimu nayo na asikinaike na kujisalimisha, basi atakosa Tawhiyd takasifu, maarifa ya kweli na imani sahihi.

MAELEZO

Yule asiyeamini yale ambayo imefichikana kwake utambuzi wake, kama vile utambuzi wa namna, bado analazimika kuyaamini na kurudisha utambuzi wake kwa Allaah (´Azza wa Jall):

فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۖ وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَيَقُولُونَ مَاذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِهَـٰذَا مَثَلًا 

”Basi wale walioamini wanajua kwamba hiyo ni haki kutoka kwa Rabb wao, ama wale waliokufuru husema: Anataka nini Allaah kwa mfano huu?”[1]

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

”Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayah zilizo wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo haziko wazi maana yake. Ama wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zisizokuwa wazi kwa ajili ya kutafuta fitina na kutafuta kupotosha [kwa kufasiri maana yake iliyojificha]; na hakuna ajuae tafsiri yake [iliyojificha] isipokuwa Allaah.”

Allaah amewaficha ujuzi wake viumbe, kwa ajili hiyo usiichoshe nafsi yako kutaka kuifikia. Kisha akasema (Subhaanah):

وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ

“Ama wale waliobobea katika elimu husema: “Tumeziamini; zote ni kutoka kwa Mola wetu”, na hawakumbuki isipokuwa wale wenye akili.”[2]

Wananyenyekea na kujisalimisha. Kutojua maana fulani hakuwazuii kuamini na kujisalimisha. Hakuwazuii vilevile kurudisha maana ya zile Aayah za Qur-aan zisizokuwa wazi kwenda katika zile Aayah zilizo wazi ili izifasiri na ibainike maana yake. Kisha wanasema:

كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا

“… zote zinatoka kwa Mola wetu.”

[1] 2:26

[2] 3:7

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 82-83
  • Imechapishwa: 23/01/2023