72. Matamshi ya Tashahhud – Tamko la Ibn Mas´uud

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafunza Maswahabah sampuli mbalimbali za Tashahhud:

1- Tashahhud ya Ibn Mas´uud. Ibn Mas´uud amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinishika mkono wangu kwa mikono yake miwili na akanifunza Tashahhud kama anavyonifunza Suurah katika Qur-aan:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah [pindi anaposema hivo basi inamgusa kila mja mwema mbinguni na ardhini]. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

Tulikuwa tukisema hivo wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yupamoja nasi. Alipofariki tukawa tunasema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.”[1]

[1] al-Bukhariy, Muslim, Ibn Abiy Shaybah (2/90/1), as-Sarraaj na Abu Ya´laa katika ”al-Musnad” (2/258). Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (321). Maneno ya Ibn Mas´uud “Tulikuwa tukisema hivo wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yupamoja nasi. Alipofariki tukawa tunasema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.”

ni dalili inayoonyesha kuwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakisema katika Tashahhud ya kwanza wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته

“Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume!”

Baada ya kufa kwake wakabadilisha matamshi na kusema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.”

Hilo pasi na shaka ni lazima liwe limetokana na kuridhia kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nadharia hiyo inaungwa mkono vilevile na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na jambo la hakika ni kuwa naye alifunza Tasahhhud kama ifuatavyo:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.” (as-Sarraaj katika ”al-Musnad” (2/1/9) na al-Mukhallas katika ”al-Fawaa-id” (1/54/11) kwa cheni mbili za wapokezi kupitia kwake)

Haafidhw Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nyongeza hii udhahiri wake ni kwamba walikuwa wakisema:

السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته

“Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume!”

wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa bado yuko hai. Alipofariki (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndipo wakaacha aina ya kumlenga na wakawa wanasema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.””

Ibn Hajar amesema vilevile:

“as-Subkiy amesema katika “Sharh-ul-Minhaaj” baada ya kutaja nyongeza hii kwa Abu ´Awaanah: “Ikiwa haya yamesihi kutoka kwa Maswahabah basi inafahamisha kwamba sio wajibu kusema kwa aina ya kumlenga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kufa kwake. Kwa hiyo mtu anaweza kusema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.””

Haya yamesihi pasi na shaka na nimepata upokezi wenye nguvu mwingine unaotilia nguvu. ´Abdur-Razzaaq amesema: “Ibn Jurayj amenikhabarisha: ´Atwaa amenikhabarisha ya kwamba Maswahabah walikuwa wakisema wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yuhai:

السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته

“Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume!”

Alipofariki wakasema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.””

Mlolongo wa wapokezi ni Swahiyh. Hata hivyo Sa´iyd bin Mansuur amepokea kupitia kwa Abu ´Ubaydah bin ´Abdillaah bin Mas´uud kutoka kwa baba yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafunza Tashahhud. Baada ya kutaja tamko Ibn ´Abbaas akasema: “Wakati bado Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko hai ndipo tulikuwa tukisema:

السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته

“Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume!”

Ndipo akasema Ibn Mas´uud: “Hivo ndivyo tulivyojifunza na hivo ndivyo tunavyofunza.”

Ni kama kwamba Ibn ´Abbaas alisema hivo kwa lengo la kuhakiki na kwamba Ibn Mas´uud hakurejea kwake. Lakini upokezi wa Abu Ma´mar [kwa al-Bukhaariy] ni Swahiyh zaidi kwa sababu Abu ´Ubaydah hakuwahi kusikia kutoka kwa baba yake. Pamoja na hivyo cheni ya wapokezi mpaka kwake ni dhaifu.”

Wanachuoni wengi wahakiki, akiwemo al-Qastwalaaniy, az-Zarqaaniy na al-Luknawiy, wameyanukuu maneno haya ya Haafidhw Ibn Hajar kwa kuyakubali bila kuyapinga. Rejea katika asili kuhusu zaida juu ya maudhui haya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 140-141
  • Imechapishwa: 30/12/2018